News

Wakaazi watishia kuandamana kufuatia uhaba wa maji Kilifi

Published

on

Wakaazi wa kaunti ya Kilifi wametishia kuandamana hadi katika ofisi za Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro kufuatia uhaba maji uliyodumu kwa takribani mwezi mmoja katika baadhi ya maeneo ya kaunti hiyo.

Wakaazi hao wakiongozwa na Kiongozi wa kidini wa Kanisa la Kibaptist kanda ya Pwani Rev. Francis Katana, walisema suala la maji ni muhimu kwa jamii za kaunti ya Kilifi na kwamba serikali ya kaunti inafaa kulichukuliwa kwa uzito suala hilo na kulitatua.

Katana anasema idadi kubwa ya wakaazi hasa wa mji wa Malindi wamekuwa wakipitia changamoto hiyo kwa mda mrefu na hata baada ya kuwasilisha lalama zao kwa idara husika ikiwemo ofisi za Kampuni ya usambazaji maji ya Malindi, MAWASCO, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo.

Kiongozi huyo wa kidini alisisitiza kwamba maandamano hayo yatafanywa kwa kuzingatia amani na kwamba wakaazi watatembea hadi katika ofisi za Gavana Mung’aro ili kuwasilisha lalama zao.

“Tumechoka na hii shida ya uhaba wa maji iliyodumu kwa mwezi mmoja sasa na tutafanya maandamano hadi kwa ofisi za Gavana ili atueleza shida iko wapi, mbona wakaazi tunahangaika na uhaba wa maji”, alisema Rev. Katana.

Viongozi hao wa kidini pamoja na wakaazi wamelalamikia kutoangaziwa kwa maslahi yao licha ya kuwasilisha lalama kwa viongozi na wawakilishi wa maeneo yao, wakisema wakati umefika sasa kwa viongozi kuwajibika ama wananchi watatumia mamlaka yao ya kidemokrasia kuwatimua kazini.

Kwa upande wake Mwanasiasa Peter Ziro aliitaka serikali ya kaunti ya Kilifi kutatua changamoto hiyo mara moja ili kuwapungumzia mahangaiko wakaazi hao, akisema serikali ya kaunti iko na raslimali za kutosha za kuzikabili changamoto zinazowakumba wananchi mashinani.

“Tunashangaa na serikali hii ya Gavana Mung’aro, yani suala la maji ambalo ni uhai kwa wananchi waliyomchagua analichukulia kama jambo la mzaa, watu wanahitaji maji kwa matumizi ya kinyumbani na tukiendelea hivi basi tutateseka. Viongozi waliopewa jukumu la kushughulia maslahi ya wananchi ni lazima wawajibike kikamilifu”, alisema Ziro.

Akijubu lalama hizo zilizoibuliwa na wakaazi hao, Mkurugenzi wa Kampuni ya usambazaji maji ya Malindi, (MAWASCO) Felix Wanje alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, akisema ilichangiwa na kukatwa kwa nguvu za umeme kutokana na deni la umeme ambalo bado halijalipwa.

“Changamoto kweli ipo na hiyo shida tunaishughulikia na wananchi watapata maji hivi karibuni. Tatizo hilo lilichangiwa na kukatwa kwa nguvu za umeme kutokana na deni ambalo bado tunadaiwa lakini tunalishughulikia suala hilo”, alieleza Wanje.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version