News
Wanaume wahimizwa kuzungumzia matatizo yanayowakabili
Mwezi wa Juni huwa umetengwa kimataifa kama mwezi wa kuhamasisha jamii kuhusu afya ya akili, huku kukiwa na msisitizo maalum wa Afya ya Akili kwa Wanaume (Men’s Mental Health Awareness Month).
Mwanzilishi wa shirika la MK initiative, Millicent Khayanga alisema wanaume wengi wanakabiliwa na hali ya msongo wa mawazo hali inayofanya baadhi yao kuchukua maamuzi mabaya kama ya kujitoa uhai.
Akizungumzia suala hilo baada ya kuongoza matembezi ya kutoa hamasa kuhusu afya ya akili kwa wanaume mjini Kilifi kaunti ya Kilifi, Millicent aliishinikiza jamii kutowachukulia kama watu wadhaifu wanapopaza sauti zao kutokana na changangomoto zinazowakabili.
“Jamii imefanya wanaume kutokuzungumzia changamoto zinazowakabili kutokana na dhana kuwa mwanamume hafai kuonyesha unyonge wake,” alisema Khayanga.
Kwa upande wa wadau wengine katika mchakato huu wa kutoa hamasa kwa wanaume kuhusu afya ya akili waliishinikiza serikali kutenga fedha maalumu za kuwawezesha wanaume kujikimu kimaisha ili kuwaepusha na hali hii.

Wanaharakati wa jamii wahimiza umuhimu wa mwezi wa kuhamasisha jamii kuhusu afya ya akili
Ni kauli ambazo ziliungwa mkono na Patrick Abio mkaazi wa Kilifi ambaye alisema ikiwa jamii itawakumbatia wanaume na kutowahukumu wanapozungumzia changamoto zinazowakabili itakuwa vyema kwani hatua hiyo itadhibiti visa vya msongo wa mawazo miongoni mwao pamoja na kuzuia visa vya kujitoa uhai.
“Ikiwa serikali, mashirika na jamii zitachukulia hili kwa uzito itakuwa afueni kubwa kwa wanaume ” Alisema Abio.
Taarifa ya Janet Mumbi