News
Washukiwa 5 wa uhalifu wanazuiliwa na polisi Likoni
Maafisa wa polisi katika eneo bunge la Likoni kaunti ya Mombasa wanawazuiliwa washukiwa 5 wa uhalifu waliokamatwa katika oparesheni iliyofanyika maeneo ya Duduz na Bufallo siku ya Jumatatu tarehe mosi Juni 2026.
Washukiwa waliokamatwa ni Brian Musa mwenye umri wa miaka 24, Abubakar Mahasi wa umri wa miaka 20, Juma Kassim mwenye umri wa miaka 16, Omar Gobeko maarufu Mboga mwenye umri wa miaka 19 na Jackson Mwambu mwenye umri wa miaka 26.
Msako huo uliongozwa na mkuu wa kituo cha polisi cha Shelly Beach pamoja na kikosi cha maafisa wa polisi.
Maafisa wa Polisi wamesema mshukiwa Brian Musa anakabiliwa na tuhuma za maandalizi ya kutenda kosa la jinai, huku Ababakar Mahasi, Juma Kassim na Omar Gobeko wakihusishwa na tuhuma za wizi wa mabavu.
Mshukiwa mwengine Jackson Mwambu anahusishwa na tuhuma za kupatikana na mali ya serikali kinyume cha sheria.
Katika oparesheni hiyo, maafisa wa polisi walifanikiwa kupata vielelezo mbali mbali ikiwemo panga tatu pamoja na koti la jeshi la KDF.
Taarifa ya Joseph Jira