News
Washukiwa wa wizi wa mabavu wakamatwa Mombasa
Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, katika eneo bunge la Kisauni kaunti ya Mombasa wanasema wamewatia mbaroni washukiwa wawili wa uhalifu wa wizi wa mabavu, waliokuwa wakihangaisha wakazi wa Kisauni na maeneo ya jirani.
Wawili hao, Chigamba Salim Dalu mwenye umri wa miaka 35 na Hassan Ndegwa Nyota mwenye umri wa miaka 27, pamoja na wengine watatu ambao bado hawajakamatwa, wanadaiwa kutekeleza uvamizi wa usiku wa manane katika nyumba moja eneo la Majaoni, Kisauni.
Kundi hilo la kihalifu liliingia kwa nguvu nyumbani humo, na kwa ukatili wakampiga risasi mwenye nyumba kabla ya kuiba runinga ya ukubwa wa inchi 75, simu mbili za mkononi, na vitu vingine vya thamani na kutokomea gizani.
Msako ulianzishwa mara moja kupitia msaada wa uchunguzi wa kielektroniki na kidijitali, na maafisa hao wakafanikiwa kumnasa Chigamba katika maficho yake eneo la Kinango, akiwa na moja ya simu zilizoibwa wakati wa tukio.
Aidha msako huo uliendelea jijini Mombasa ambako polisi walifanikiwa kumnasa Hassan.
Washukiwa hao wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Taarifa ya Mwanahabari wetu