News
Waziri Deborah awahimiza wakenya kupanda miti kwa wingi
Serikali imewahimiza wakenya kutumia fursa ya siku ya kitaifa ya mapumzo ya Mazingira Oktoba 10, na kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi na kupanda miti ili kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.
Waziri wa Mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu nchini Deborah Barassa alisema kila mkenya ana jukumu la kutembelea shule za msingi aliyosomea na kutekeleza jukumu lake la kupamba miti.
Deborah alisema hatua hiyo itasaidia pakubwa taifa la Kenya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi sawa na kuafikia azma ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka wa 2030.
“Tuko na malengo ya kuhakikisha tunatunza mazingira na hii itafaulu ikiwa tutapanda miti kwa wingi hasa kila mmoja atumie siku ya mazingira na kutembelea shule tumesoma na kupanda miti ili kudhibiti mazingira”, alisema Deborah.
Kwa upande wake Afisa mkuu mtendaji wa Taasisi ya utafiti wa misitu nchini KEFRI Jane Njuguna, amesema maeneo mengi nchini yanakabiliwa na kiangazi kikali kutokana na uhaba wa misitu, akisisitiza haja ya wakenya kutumia siku hiyo kupanda miti.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi