Sports

Harambee Stars Wapiga Ushelisheli Kasarani, Olunga Asawazisha Rekodi ya Oliech

Published

on

Timu ya soka Harambee Stars hatimaye wamehitimisha kusubiri ushindi wa nyumbani kwenye kufuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kushinda kwa kishindo cha mabao 5-0 dhidi ya UShelisheli katika uwanja uliojaa mashabiki wa Kasarani Jumanne alasiri.

Kocha mkuu Benni McCarthy alifanya mabadiliko sita kutoka kwa kikosi kilichopoteza 3-1 dhidi ya Gambia wiki iliyopita. Kipa Brian Bwire alimchukua nafasi Byrne Omondi langoni, huku Ronney Onyango akibaki beki wa kulia.

Kwa kuwa Aboud Omar alikuwa amesimamishwa, Manzur Okwaro alicheza katika nafasi yake ya asili kama beki wa kushoto mabadiliko yaliyokaribishwa baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika michuano ya CHAN 2024 kama kiungo mkabaji. Kwenye moyo wa safu ya ulinzi, Sylvester “Sili” Owino na Collins Shichenje waliendeleza ushirikiano wao, wakilindwa na Alpha Chris Onyango, aliyemchukua nafasi Richard Odada. Aliungana na Duke Abuya katikati ya uwanja, huku Ryan-Wesley Ogam akichukua nafasi ya Timothy Ouma Noor, akicheza kama namba tisa ya uongo.

Job Ochieng’, aliyeng’aa alipoingia kama mchezaji wa akiba dhidi ya Gambia, alianza kwenye wingi wa kushoto mbele ya Emmanuel Osoro, huku Wilson Lenkupae anayekipiga Australia akicheza wingi wa kulia. Nahodha Michael Olunga aliongoza safu ya mashambulizi.

Mashabiki hawakungojea kwa muda mrefu. Dakika ya 7, nyota wa moto Ogam alivunja kimya kwa kumalizia kwa ustadi.

Kenya walimiliki mpira na kuongeza bao la pili dakika ya 35 kupitia Collins Shichenje aliyemalizia pasi ya Abuya. Dakika tatu baadaye, Ogam alifunga tena — bao lake la nne katika mechi sita pekee — na kufanya matokeo kuwa 3-0. Kabla ya mapumziko, Olunga alifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Ogam kuangushwa ndani ya kisanduku, na kuwapa Stars uongozi wa 4-0 kipindi cha kwanza.

Bao hilo lilimfanya Olunga kufikia rekodi ya Dennis Oliech ya mabao 34, na kumfanya awe mfungaji wa pili bora wa muda wote wa Kenya kwa pamoja.

Kipindi cha pili, McCarthy aliwatoa Ochieng’, Lenkupae na Abuya na kuwaingiza Ben-Stanley Omondi, Boniface Muchiri na Marvin Nabwire. Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika ya 68, Olunga aliporuka juu na kufunga kwa kichwa kutoka krosi safi ya Onyango, na kuhitimisha ushindi wa 5-0.

Licha ya Kenya kutokuwa na nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Kanada na Mexico, ushindi huu uliwaweka katika nafasi ya nne Kundi F wakiwa na pointi 9 — moja nyuma ya Burundi na mbili juu ya Gambia, waliotarajiwa kukutana usiku huo. Stars sasa wanageuza macho yao kwenye mechi za mwisho za kufuzu mwezi Oktoba, ambapo watakutana na Burundi (Okt 6) na vinara wa kundi Ivory Coast (Okt 13).

Ivory Coast kwa sasa wanaongoza kundi wakiwa na pointi 19, wakiwa pointi moja mbele ya Gabon walioko nafasi ya pili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version