News
Bunge la seneti kujadili hoja ya kutimuliwa kwa Gavana Mutai
Bunge la seneti limetangaza kwamba siku ya Jumatano Agosti 20, 2025 litakuwa na kikao maalum cha bunge ili kujadili hoja mbili muhimu kwa kuambatana na sera za bunge.
Katika notisi ya gazeti rasmi la serikali, kikao cha kwanza itakuwa shughuli ya kuapishwa kwa Seneta mteule Consolata Nabwire ili kuchunua nafasi ya aliyekuwa seneta mteule Gloria Orwoba aliyetimuliwa mamlakani.
Kikao cha pili kitakuwa cha kujadili hoja ya kubanduliwa mamlakani kwa Gavana wa Kericho Dkt Eric Kipkoech Mutai, kikao ambacho kimeratibiwa kuanza rasmi mwendo wa saa nane alasiri.
Gavana Mutai, anakabiliwa na shutma za ufisadi, utumizi mbaya wa raslimali za umma, ukiukaji wa Katiba pamoja na kujinufaisha binafsi na miradi ya umma.
Maseneta hao hata hivyo baada ya kujadili hoja hiyo na kusikiza pande zote mbili, bunge la seneti litaamua kumnusuru Gavana Mutai ama kumtimua mamlakani.
Tayari Kenya ina magavana watatu waliotimuliwa uongozi kupitia kura ya kutokuwa na Imani nao baada ya Wawakilishi wadi kutofautiana na magavana wao huku wengine wakipatikana na sakata za ufisadi na ukiukaji wa katiba.
Iwapo Gavana Mutai atatimuliwa mamlakani basi atakuwa anaongeza idadi ya magavana waliotemwa na Wawakilishi wadi kufikia Magavana wanne, akiwemo aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko, aliyekuwa Gavana wa Embu Kawira Mwangaza na Gavana Mutai iwapo hatapokea shoka la kutimuliwa uongozini.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi