Sports
Cape Verde Yashangaza Cameroon, Yakaribia Kufaulu kufuzu Kombe la Dunia kwa Mara ya Kwanza
Visiwa vya Cape Verde, taifa dogo la kisiwa Afrika Magharibi lenye idadi ya watu wasiozidi 550,000, iliishinda Cameroon 1-0 siku ya Jumanne na kuimarisha matumaini ya kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Timu hiyo kwa jina la utani Blue Sharks wanahitaji alama tatu mwezi Oktoba kutoka mechi dhidi ya Libya na nyumbani dhidi ya Eswatini ili kushinda Kundi D, ambalo lilitarajiwa kudhibitiwa na Cameroon waliowahi kufuzu Kombe la Dunia mara nane.
Mshambuliaji anayekipiga Italia, Dailon Livramento, mwenye umri wa miaka 24 aliyezaliwa Rotterdam kwa wazazi wa Cape Verde, ndiye aliyeibuka shujaa mjini Praia baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 54. Hilo lilikuwa bao lake la tatu katika kufuzu Kombe la Dunia 2026, baada ya mabao mawili yaliyoiwezesha Cape Verde kupata ushindi wa kushtua dhidi ya Angola Machi iliyopita.
Ushindi dhidi ya Cameroon ulikuwa wa furaha zaidi baada ya Indomitable Lions kushinda 4-1 walipokutana Yaoundé mwaka jana.
Cape Verde wana pointi 19, nne mbele ya Cameroon, ambao watakabiliana na Mauritius ugenini na kisha kuwakaribisha Angola katika raundi mbili za mwisho za mchujo wa kufuzu ulioanza mwaka 2023.
Cameroon, ambao wamefuzu mara nane kwenye michuano ya dunia (rekodi ya Afrika), walipata pigo mara mbili kwani sasa wameshuka hadi nafasi ya tano miongoni mwa timu zilizoshika nafasi ya pili. Ni timu nne pekee zilizoshika nafasi ya pili zenye rekodi bora ndizo zitakazofuzu kwa mchuano mdogo, ambapo mshindi ataenda kucheza mchujo wa mabara mwezi Machi kwa nafasi mbili za Kombe la Dunia.
Kwa Cape Verde, kuwa ukingoni mwa kufuzu kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia ni mabadiliko makubwa, baada ya kushika mkia kwenye kundi la kufuzu AFCON 2025 kwa kushinda mechi moja pekee kati ya sita.
Kocha wa timu hiyo Pedro Leitao Brito, anayejulikana kwa jina maarufu Bubista (miaka 55), amekuwa akiinoa timu ya taifa tangu 2020. Nahodha ni mshambuliaji anayecheza Uturuki Ryan Mendes, mwenye miaka 35.
Cape Verde wanashikilia nafasi ya 73 duniani, nafasi 22 nyuma ya Cameroon waliowahi kuwa mabingwa wa Afrika mara tano. Mafanikio yao bora ya kimataifa ni kufika robo-fainali ya AFCON mwaka jana.
Senegal walipindua meza
Senegal walipindua matokeo kutoka nyuma kwa mabao mawili na kushinda DR Congo 3-2 mjini Kinshasa, na kuongoza Kundi B kwa tofauti ya pointi mbili.
Cedric Bakambu na sajili mpya wa Newcastle United Yoane Wissa waliwafungia wenyeji kabla ya kurejea kwa nguvu kwa Senegal katika kipindi cha pili, kilichoisha kwa kiungo wa Tottenham Pape Matar Sarr kufunga bao la ushindi.
Ushindi wa Senegal dhidi ya Sudan Kusini ugenini na nyumbani dhidi ya Mauritania mwezi Oktoba utawapa tiketi ya tatu mfululizo ya Kombe la Dunia.
Nigeria matatani
Nigeria wako hatarini kukosa Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya vinara wa Kundi C Afrika Kusini mjini Bloemfontein.
Mabeki wa Super Eagles walifunga mabao yote mawili kipindi cha kwanza: nahodha William Troost-Ekong akijifunga, kisha Calvin Bassey kusawazisha kwa kichwa.
Nigeria wako nyuma ya Afrika Kusini kwa pointi sita, na matumaini yao ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 Amerika Kaskazini huenda yakategemea kumaliza nafasi ya pili na kufuzu mchujo.
Misri wasubiri kidogo
Ushindi ungeihakikishia Misri kufuzu kutoka Kundi A, lakini walilazimishwa sare ya 0-0 na Burkina Faso walioko nafasi ya pili. Pharaohs wanahitaji pointi mbili zaidi kufanikisha kufuzu kwa mara ya nne.