News

Gavana Sakaja aponea shoka la kutimuliwa mamlakani

Published

on

Mchakato wa kumbandua mamlakani Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja pamoja na Naibu wake James Muchiri umekosa kuendelea baada ya Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga kuingilia kati mchakato huo.

Hii ni baada ya Odinga pamoja na viongozi wakuu wa chama cha ODM na Wawakilishi wadi wa kaunti ya Nairobi kufanya kikao cha mazungumzo kwa masaa kadhaa na kuibuka na suluhisho la kusitishwa kwa mchakato huo.

Akizungumza na Wanahabari baada ya kikao hicho kilichoandaliwa jijini Nairobi, Mbunge wa Makadara George Aladwa alisema kikao hicho kimasikiliza lalama zote zilizoibuliwa na wawakilishi wadi hao dhidi ya Gavana Sakaja na kuafikia masuala kadhaa.

Aladwa alisema Gavana Sakaja amehimizwa kurekebisha masuala yalioibuliwa na Wawakilishi wadi hao sawa na kushirikiana naoi li kuhakikisha kaunti ya Nairobi inapiga hatua kimaendeleo na wananchi wa kaunti hiyo wananufaika.

Siku ya Jumatatu Septemba 1, 2025, Wawakilishi wadi hao wa Nairobi wakiongozwa na Mwakilishi wadi ya Kileleshwa Robert Alai, walisema Gavana Sakaja alishindwa kuwajibikia majukumu yake kama Gavana na kwamba hafai kushikilia wadhfa huo.

Wawakilishi wadi hao waliorodhesha malalamishi zaidi ya 20 dhidi ya Gavana Sakaja ikiwemo uongozi duni, ukiukaji wa Katiba, usimamizi duni wa jiji la Nairobi, kuporomoka kwa majengo kiholela, mirundiko ya taka katikati wa jiji, huduma duni za afya, miongoni mwa masuala mengine.

Wawakilishi wadi hao walisema wako na ushahidi wa kutosha dhidi ya Gavana Sakaja, wakishikilia kwamba Gavana huyo ameshindwa kusimamia jiji la Nairobi, wakipendekeza kutimuliwa Mamlakani pamoja na Naibu wake James Muchiri.

Itakumbukwa kwamba Wawakilishi wadi zaidi ya 100 walikuwa tayari wametia saini hoja ya kumbandua mamlakani Gavana Sakaja pamoja na Naibu wake James Muchiri kwa madai ya kushindwa kuwajibikia majukumu yao miongoni mwa hoja zengine zaidi ya 20 lakini hatua ya Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga kuingilia kati suala hilo kulimnuru Gavana Sakaja.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version