News
Gavana Sakaja taabani kuhusu hoja ya kubanduliwa mamlakani
Zaidi ya Wawakilishi wadi 70 wa kaunti ya Nairobi walitia saini hoja ya kutokuwa na Imani na Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja, ambayo inalenga kumbandua mamlakani iwapo hoja hiyo itapitishwa na bunge hilo.
Katika kikao cha siku ya Jumanne Agosti 25, 2025 katika bunge hilo ambacho kilihudhuriwa na Wawakilishi wadi 96 kati ya 122, Wawakilishi wadi hao walitia saini hoja hiyo ambayo pia inalenga kumtema nje Naibu Gavana wa kaunti hiyo James Muchiri.
Kikao hicho kilichoongozwa na Spika wa bunge hilo Ken Ng’ondi pamoja na kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo Peter Imwatok, Niabu Kiranja wa wachache katika bunge hilo Mark Mugambi na Waithera Chenge, kimeweka wazi ajenda za kumtimua Gavana Sakaja na Muchiri.
Wawakilishi wadi hao walisema Gavana Sakaja pamoja na Naibu wake walishindwa kusimamia vyema raslimali za kaunti, ukiukaji wa Katiba, utumizi mbaya wa ofisi ya umma miongoni mwa masuala mengine ibuka.
Iwapo hoja hiyo itafaulu katika mchakato wa kumtimua Gavana Sakaja na naibu wake, basi moja kwa moja spika wa bunge hilo Ken Ng’ondi atachukua nafasi ya ugavana kwa kipindi cha siku 60 kabla ya uchaguzi wa ugavana kufanyika.
Hayo hayo yatategemea iwapo hoja hiyo itapitishwa katika bunge hilo baada ya Wawakilishi wadi wa Nairobi watakaporejelea vikao vya bunge mwezi Septemba na iwapo bunge la Seneti kwa kuzingatia kanuni za Katiba itaidhinisha hoja hiyo ya Wawakilishi wadi.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi