News

Kaunti ya Kilifi yasambaza tani 62.5 za Unga wa uji kwa shule za ECDE

Published

on

Serikali ya kaunti ya Kilifi yaendeleza mpango wa kusambaza tani 62.5 za unga wa uji ulioimarishwa kwa virutubisho kwa vituo 813 vya umma vya ECDE, hatua itakayowanufaisha zaidi ya wanafunzi wa chekechea 50,000 katika kaunti nzima ya Kilifi.

Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Maitha Mung’aro alisema mpango huo wa chakula pekee ni kati ya juhudi za kuhakikisha kila mtoto anapata lishe hasa akiwa shuleni.

Mung’aro amebainisha kupitia mtandao wake wa Facebook kwamba magari ya mizigo tayari yameelekezwa katika kaunti ndogo zote saba, yakigusa wadi zote 35 ili kuhakikisha kila kituo cha ECDE kinapokea mgao wake bila kuchelewa.

Katika Kituo cha chekechea kilichopo Fumbini, Wadi ya Kibarani, kaunti hii ya Kilifi gavana Mung’aro amesema maafisa wa kaunti walikagua shehena hiyo kama sehemu ya uzinduzi wa usambazaji. Ukaguzi huu uliashiria dhamira ya serikali ya kaunti katika uwajibikaji, uwazi na ustawi wa wanafunzi.

Maafisa kutoka Idara ya Elimu na idara ya Teknolojia na Mawasiliano ICT walibainisha kuwa mpango huu wa unga wa uji wenye virutubisho umebuniwa ili kuboresha lishe, mahudhurio shuleni, na umakini wa wanafunzi wa ECDE.

Serikali ya Kaunti ya Kilifi, kupitia Idara ya Elimu na ICT, itaendelea kuimarisha mpango wa chakula cha ECDE kama sehemu ya juhudi zake za kuendeleza elimu bora na ustawi wa mtoto katika kaunti ya Kilifi.

Taarifa ya Elizabeth Mwende

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version