Sports

Kikosi Cha Voliboli Malkia Strikers Kina Mortisha Kuelekea Mechi Ya Pili Dhidi ya Poland

Published

on

Kocha wa timu ya taifa ya mpira wa voliboli ya akina dada, Malkia Strikers, Geoffrey Omondi, ana matumaini makubwa kuelekea mechi yao ya pili ya Kundi “G” dhidi ya Poland katika Mashindano ya Dunia ya FIVB yanayoendelea Phuket, Thailand, leo jioni.

Kenya siku ya Jumamosi ilipoteza kwa seti za moja kwa moja (22-25, 08-25, 20-25) dhidi ya Ujerumani katika mechi ya ufunguzi wa makundi.

Akizungumza baada ya mazoezi ya Jumapili, Omondi alisema iwapo wachezaji wake wataendelea kutoka pale walipoishia Jumamosi, wanaweza kushangaza Poland, ambayo inashikilia nafasi ya tatu kwenye viwango vya dunia vya FIVB.

“Wachezaji walifanya kazi nzuri sana walipocheza na Ujerumani, na tunatumaini watakuwa na ari ileile watakapomenyana na Poland. Tumefanya mazoezi mazuri na kurekebisha maeneo tuliyolegea dhidi ya Ujerumani. Ninaamini tunaweza kusababisha mshangao dhidi ya Poland. Wachezaji wako na morali ya juu baada ya baadhi yao kulipwa posho zao, na sasa umakini uko kwenye mechi zilizobaki,” alisema Omondi, ambaye pia ni kocha wa Kenya Pipeline, mabingwa wa Ligi ya Taifa ya Shirikisho la Mpira wa Wavu Kenya (KVF).

“Iwapo tunaweza kushinda seti moja au mbili au hata kushinda mechi kabisa, basi hiyo itakuwa hatua kubwa. Timu hii ina uwezo wa kushindana katika kiwango cha juu iwapo watapata mechi nyingi za kirafiki za kimataifa kama tulizocheza kabla ya mashindano. Hii yote inalenga maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya 2028,” aliongeza.

Kenya wiki iliyopita ilicheza mechi za kirafiki dhidi ya Uhispania na wenyeji Vietnam na kupoteza zote. Mabingwa wa Afrika hao watakamilisha michezo ya makundi Jumatano kwa kukutana na Vietnam.

Timu mbili za juu mwishoni mwa michezo ya awali zitafuzu kuingia raundi ya pili.

Nahodha wa Malkia Strikers, Meldina Sande, alithibitisha kuwa baadhi ya wachezaji wamelipwa posho zao baada ya timu kulalamika awali kuwa serikali haijawalipa kwa wakati.

“Tunashukuru Wizara ya Michezo, Kamati ya Olimpiki ya Taifa la Kenya (NOC-K) kwa msaada wake. Sasa tuko tayari kushindana na kupata matokeo mazuri. Tunawashukuru Wakenya walioko nyumbani kwa sapoti yao, na tunawaombea tuwape furaha,” alisema Sande, ambaye anachezea Rwanda Police.

Kenya itacheza mechi ya mwisho Jumatano dhidi ya Vietnam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version