News

Naibu rais akosoa upinzani kuhusu bei ya mafuta nchini

Published

on

Naibu rais Profesa Kithure Kindiki amerejea tena kaunti ya Kilifi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuendeleza ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika kanda ya Pwani.

Hata hivyo ziara hiyo imeonekana kuangazia zaidi suala tata la kupanda kwa bei ya mafuta nchini ambalo linadaiwa kusababishwa na vita vinavyoendelea katika mashariki ya Kati.

Akitetea hatua ya serikali, naibu rais alisema tayari serikali imechukua hatua madhubuti na za haraka kupunguza ushuru wa mafuta, ili kumkinga mwananchi kutokana na athari za mfumuko wa bei za bidhaa na kuongezeka kwa gharama ya maisha.

Akihutubiwa wananchi katika eneo bunge la Rabai, Professa Kindiki alionekana kuulenga upinzani kwa kuingiza siasa katika suala la mafuta, akikosoa mpango wao wa kuandaa maandamano akisema sio suluhu kwa tatizo hilo.

Hatua ya hii ya Kindiki ilionekana kupokea msukumo kutoka kwa viongozi wakuu ndani chama cha UDA wakiongozwa na katibu wa Chama Omar Hassan Sarai ambaye alikosoa mpango ya upinzani kuandaa maandamano.

Jumatano ya aprili 15, 2026, Rais William Ruto alitangazi mipango ya serikali kutatua tatizo la kupanda kwa bei ya mafuta nchini kwa kupunguza ushuru wa mafuta.

Viongozi wengine walioandamana na naibu rais katika eneo bunge la Rabai akiwemo mwenyekiti wa bodi ya barabara nchini Aisha Jumwa, mbunge wa eneo hilo Kenga Mupe vile vile mwenyekiti wa bodi ya hazina ya michezo, sanaa na maendeleo Wakili George Kithi, waliitaka serikali kuangazia masuala mbali mbali yanayowakumba wakaazi wa kilifi, ikiwemo uhaba wa maji safi, ukosefu wa dawa hospitalini na uvamizi wa ndovu kwa wakaazi wa eneo bunge la Ganze.

Awali naibu rais alitembelea miradi mbali mbali eneo hilo ikiwemo uzinduzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu, na nyumba za malazi kwa wanafunzi wa taasisi ya ufundi, na ukaguzi wa mradi wa kituo cha huduma eneo la Shikaadabu huko Rabai.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version