News
NPSC hatimaye yatangaza kuajiri maafisa 10,000 wa polisi
Tume ya kitaifa ya huduma ya polisi (NPSC) hatimaye imetangaza usajili wa maafisa 10,000 wa polisi, na kumaliza mzozo wa muda mrefu kati yake na huduma ya kitaifa ya polisi (NPS).
Katika notisi iliyochapishwa katika gazeti moja la kila siku nchini, NPSC ilialika waenye nia ya kutuma maombi kupakua fomu za uajiri mtandaoni, kuzijaza, na kujiwasilisha katika vituo vilivyoteuliwa ili kuzingatiwa.
Zoezi hilo la nchi nzima limepangwa kuanza Oktoba 3 hadi Oktoba 9, 2025, katika vituo 416 vya usajli.
Zoezi hilo litalenga raia wa Kenya walio na umri wa kati ya miaka 18 na 28, walio pata alama ya chini ya D+ katika cheti cha mtihani wa kitaifa wa shule za sekondari (KCSE).
Kulingana na taarifa iliyotiwa saini na afisa mkuu mtendaji wa NPSC Peter Leley, wanaotuma maombi lazima wawasilishe vyeti halisi vya masomo na vitambulisho vyao vya kitaifa katika vituo vya kuajiri.
Tangazo hilo linafuatia wiki za mvutano kati ya NPSC na NPS kuhusu mchakato wa kuajiri.
Tume hiyo hapo awali ilishinikiza kuwepo kwa mtindo mpya unaohitaji waliotuma maombi kuorodheshwa kabla ya kuhudhuria zoezi la uhakiki.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilitupiliwa mbali, na kuruhusu wote waliotuma maombi hayo kujiwasilisha siku ya usajili wakiwa na fomu zilizojazwa ipasavyo.
Taarifa ya Joseph Jira