News
Nyamu: Jamii ni lazima ielemishwe kuhusu haki zao
Mwanasayansi na mkurugenzi mkuu wa shirika la kaungazia masuala ya Ndovu Jim Justus Nyamu pamoja na wanaharakati wa masuala ya wanyamapori wametoa wito kwa serikali pamoja na wadau husika kuhakikisha jamii zinaelimishwa kuhusu haki zao za namna ya kupata fidia kutokana na athari za wanyamapori.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari huko Mombasa, Nyamu alisema visa vya wanyamapori kuharibu mimea na hata kusababisha vifo na majeraha vimekuwa vikiendelea huku wananchi wengi wakikosa kufahamu taratibu za kufidiwa.
Nyamu pia alisema kunapaswa kuwa na hamasa za mara kwa mara, vijijini na maeneo ambayo yako karibu na hifadhi za wanyamapori ili wananchi wafahamu hatua ambazo wanapaswa kuchukua wanapopata hasara zinazosababishwa na wanyamapori.
Vilevile, Nyamu alitoa wito kwa serikali kuu kupitia wizara husika kuimarisha mfumo wa kulipa fidia kwa kuhakikisha unakuwa wa haraka, uwazi na haki kwa kila mmoja ambaye ameathiriwa na wanyamapori.
Naye Kamishna wa kaunti ya Mombasa Mohamed Noor alisema serikali iko tayari kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kijamii ili kuwaelimisha Wakenya kuhusu haki zao na pia kuimarisha mfumo wa utoaji wa fidia kwao.
Taarifa ya Janet Shume