News
Polisi wanasa magunia 12 ya bangi Malindi
Maafisa wa kukabiliana na dawa za kulevya Malindi katika kaunti ya Kilifi kwa ushirikiano na maafisa wa kitengo maalum cha oparesheni SOG kilicho katika kizuizi cha polisi daraja la Sabaki, wamekamata gari aina ya Toyota SUV likiwa limejaa dawa za kulevya aina ya bangi.
Maafisa hao walisema walikuwa na taarifa muhimu kuhusu gari hilo lililokuwa likisafirisha mzigo huo haramu ambapo waliweka mtego wa kusimamisha gari hilo katika eneo la Gede ila dereva alikaidi amri ya kusimama.
Ilisemekana badala yake aliongeza mwendo akigeukia barabara ya Jacaranda kutoka Kijiwetanga katika jaribio la kutoroka.
Msako mkali uliendeshwa na baada ya saa chache gari hilo lilipatikana likiwa limeachwa eneo la Mayungu nambari zake za usajili zikiwa zimebadilishwa haraka katika harakati za kuwapotosha maafisa wa upelelezi.
Baada ya ukaguzi maafisa walibaini kuwa gari hilo lilikuwa na magunia 12 ya bangi, mzigo unaokisiwa kuwa na thamani ya mamilioni ya pesa, na ambao ulikuwa ukielekezwa mitaani.
Taarifa ya Joseph Jira