News
Polisi wawarai wananchi kuwa makini dhidi ya wachungaji potovu wa kidini
Idara ya usalama kaunti ya Kilifi imewarai wakaazi kuwa waangalifu dhidi ya Wachungaji potovu waliojitokeza na kuwapotosha wananchi kwa misingi ya kidini.
Afisa mkuu wa idara ya upelelezi wa jinai DCI katika kaunti ya Kilifi Robert Kiinge, alisema itikadi potovu za kidini itakomeshwe iwapo wananchi watakuwa mstari wa mbele kuwaripoti watu wanaowashuku kuwa na itikadi hizo.
Katika kikao na Wanahabari ofisini mwake mjini Kilifi, Kiinge aliwarai wazazi na jamii kwa jumla kufuatilia mienendo ya watoto ili kuzuia kupotoshwa katika itikadi za kidini, akisema kuna haja ya jamii kuwa makini.
“Kuna chipuza watu ambao wanapatiana mafunzo ya kidini ambazo haziandamani na mahubiri ambayo sisi tunajua, naomba mkiona mtu ambaye anaendeleza maneno ambayo hayaandamana na mafunzo ya vitabu tafadhali walete kwenye ofisi za usalama”, alisema Kiinge.
Wakati huo huo amedokeza kwamba vitengo mbalimbali vya kiusalama viko mashinani kuendeleza oparesheni za kijasusi ikiwemo kwa viongozi wa kidini kuhusu vyeti vyao wa masomo ya thiolojia na stakabadhi waliozo nazo ili kudhibiti mafundo potovu.
Kauli yake imejiri baada ya Mchungaji Kamanza Mwatela wa kanisa la Jesus Ministry kuzuiliwa na maafisa wa polisi kwa tuhma za kuendeleza itikadi potovu za kidini sawa na washukiwa kadhaa wanaohusishwa na mauaji ya watu katika kijiji cha Kwa Binzaro eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi