News
Odinga awaalika wakenya kwenye kumbukumbu za Sabasaba
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amewaalika wakenya kujumuika naye kati kumbukumbu za maandamano ya siku ya Sabasaba katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi.
Odinga alisema hatua hiyo ni kuwakumbuka wale waliopigania mfumo wa vyama vingi nchini ambao kulingana naye mfumo huo ulifaulu japo bado kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kulainishwa.
Itakumbukwa kuwa Odinga alikuwa miongoni mwa waliopanga siku ya maandamano ya Sabasaba ya kwanza nchini, mnamo Julai 7, 1990.
Odinga alisema yuko tayari kuadhimisha miaka 35 ya siku hii.
Kinara huyo wa ODM alisema uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi umebeba historia ya kipekee kutokana na matukio ya wakati huo, ambapo waliowasili katika Sabasaba ya kwanza walikabiliwa na maafisa wa usalama, baadhi walipoteza maisha na mamia wakijeruhiwa katika vita vya kupigania siasa za vyama vingi.
Wakati huo huo kundi la wahuni lilivamia kikao kilichokuwa kikihutubiwa na makundi ya kinamama katika ofisi za tume ya kutetea haki za kibinadam KHRC Jijini Nairobi jumapili 6, Julai 2025.
Kinamama hao walikuwa wamewasili katika ofisi za tume hiyo ili kuzungumzia siku ya Sabasaba na walilazimika kusitisha kikao hicho huku mali na bidhaa nyingine muhimu zikiibwa.

Baadhi ya wanawake waliovamiwa katika makao makuu ya tume ya KHRC Nairobi
Wanahabari waliokuwa sehemu hiyo pia walivamiwa na kukimbilia usalama wao huku kinamama hao wakilazimika kuandaa kikao hicho sehemu tofauti baadaye.
Hata hivyo tume hiyo ya KHRC ililaani tukio hilo na kumtaka inspekta jenerali wa polisi nchini Douglas Kanja kufanya uchunguzi na kuwakamata waliohusika na uvamizi huo
Taarifa ya Joseph Jira