News
Rigathi Gachagua arejea nchini kutoka Marekani
Kinara wa Chama cha DCP Rigathi Gachagua amewasili nchini Kenya baada ya ziara yake ndefu nchini Marekani.
Vurugu zilishuhudiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta –JKIA ambapo wafuasi wake walimiminika katika jumba hilo huku wakiimba jina lake wakati walipokuwa wakimsubiri kupita kizuizi hicho.
Kisha alisindikizwa katikati ya umati na timu yake ya usalama hadi kwenye msafara wake uliokuwa ukimsubiri.
Wafuasi wake walikuwa wamekita kambi katika uwanja wa ndege kuanzia mapema Alhamisi asubuhi.
Gachagua alikuwa nchini Marekani kwa muda wa wiki sita, ambapo aliwakusanya wafuasi wake na kufanya mikutano ya hadhara na wakenya wanaoishi nje ya nchi.
Pia alidumisha ukosoaji mkali dhidi ya utawala wa rais William Ruto kwa shutma za ufisadi, mauaji ya kiholela na ukiukaji wa haki za binadamu.
Anatarajiwa kuongoza msafara hadi katika viwanja vya Kamukunji kwa mkutano wa hadhara, hatua ambayo serikali iliahidi kufuatilia ili kuzuia uvunjaji wa sheria.
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen alisema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake iwapo kutashuhudiwa ghasia na usumbufu.
Taarifa ya Joseph Jira