News
Ripoti ya upasuaji wa maiti yabainisha kilichomuua polisi,Haiti
Upasuaji wa maiti ya Kennedy Mutuku Nzuve afisa wa polisi aliyefariki nchini Haiti umebaini kuwa alifariki kutokana na majeraha yanayoambatana na ajali ya barabarani.
Upasuaji wa mwili ulifanyika siku moja baada ya mwili wa afisa huyo kurejeshwa nchini Kenya kutoka nchini Haiti.
Mwili wa afisa huyo ulipokewa na familia yake katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA jijini Nairobi mwendo wa saa tatu jioni siku ya Ijumaa Septemba 26, 2025.
Nzuve alifariki Agosti tarehe 31 kwenye doria ya usalama nchini Haiti, na sasa familia yake inasema hatua ya mwili wa Nzuve kurejeshwa nchini imeleta afueni.
Nzuve ni miongoni mwa maafisa watatu wa polisi wa Kenya waliofariki wakiwa kwenye oparesheni nchini Haiti, katika mpango wa kimataifa wa usaidizi wa usalama unaoungwa mkono na umoja wa kimataifa.
Awali kuliibuka mkanganyiko kuhusu hatma ya afisa mwengine wa polisi Benedict Kabiru ambaye alikuwa miongoni mwa mafisa waliopelekwa nchini Haiti.
Mkuu wa sheria aliiambia mahakama kuwa hana ufahamu kuwa afisa huyo wa polisi alifariki dunia nchini Haiti, kinyume na matamshi ya rais William Ruto katika kikao cha baraza la umoja wa mataifa jijini New York nchini Marekani.
Kabiru, aliyetumwa nchini Haiti chini ya ujumbe wa msaada wa usalama wa kimataifa (MMS) alishukiwa kuuawa na magenge yenye silaha mnamo mwezi machi 2025.

Maafisa wa polisi wa Kenya wakishika doria nchini Haiti.(picha kwa hisani)
Miezi kadhaa baadaye, huduma ya kitaifa ya polisi nchini ilikuwa bado haijathibitisha kifo chake, ikisema juhudi za kumtafuta zingali zinaendelea.
Familia ilifika mahakamani ikitaka maelezo, ikidai maelezo hayo alizuiliwa na maafisa kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu.
Mawakili wanaowakilisha familia hiyo, Jumatano 25, Septemba 2025, waliambia mahakama kwamba kukiri hadharani kwa Rais William Ruto kuwa Kabiru alikuwa miongoni mwa maafisa waliofariki Haiti, kunachukuliwa kuwa ushahidi.
“Ikiwa taarifa ya rais ni sahihi, basi inatupilia mbali ombi la habari kwa kuwa uthibitisho tayari umefanywa katika ngazi ya juu,” mahakama ilisikiza.
Wakati rais Ruto alitoa taarifa kwa umma katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, Mwanasheria mkuu alisisitiza kuwa haijapokea taarifa kama hizo kutoka kwa utawala wa polisi.
Mkanganyiko huu, walalamishi walipinga na kusema ni madai ambayo yanahitaji ufafanuzi wa haraka.
Hata hivyo mkuu wa sheria aliomba muda zaidi ili kupata taarifa zaidi.
Taarifa ya Joseph Jira