News
Serikali yahimizwa kuwachunguza viongozi wa kidini wa itikadi potovu
Kutokana na kuongezeka kwa mafundisho ya itikadi potovu katika madhehebu mbalimbali nchini, sasa serikali imehimizwa kuanza kuwatathmini upya na kuwachunguza wachungaji wote nchini.
Aliyekuwa Mwakilishi wadi ya Gongoni kaunti ya Kilifi Albert Kiraga alitoa tahadhari kwa serikali, akisema ni lazima ilifikirie upya suala hilo kwani linatishia maisha ya jamii nyingi kutokana na matukio ya kutisha katika kijiji cha Kwa Binzaro kaunti ya Kilifi.
Kiraga alizitaka asasi za kiusalama pamoja na mamlaka zengine nchini kuanzisha mchakato mpya wa kuwachunguza wachungaji wote nchini iwapo stakabidhi zao za kidini zinaambatana na mafundisho wanayotoa kwa waumini wao.
Akizungumza na Wanahabari, Kiraga alisema tukio la hivi majuzi katika msitu wa Shakahola na kijiji cha Kwa Binzaro na sasa katika eneo la Kaloleni ambapo mtu mmoja aliyejiita Kasisi alionenkana akicheza densi juu ya mti huku waumini wakigaagaa kwenye matope wakiimba na kupiga makofi.
Kwa upande wake Mhubiri Dkt Dorcas Chebet Juma, ambaye pia ni Mhadhiri wa chuo kikuu cha Pwani alisisitiza umuhimu wa elimu ya dini miongoni mwa wachungaji na ujuzi wa kidini kwa waumini, akisema hatua hiyo itakomesha itikadi za kidini na mafunzo potovu.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi