News
Vita dhidi ya dhulma za kijinsia vyaendelezwa Kilifi
Visa vya ukatili wa kijinsia (GBV), dhidi ya wanawake na watoto katika kaunti ya Kilifi vinapoendelea kushuhudiwa, mikakati ingali inaendelezwa katika kuhakikisha vinadhibiti vilivyo.
Akizungumza baada ya kuzindua mchakato wa kuhamasisha jamii kuhusu visa hivyo, mwanaharakati na pia mwanzilishi wa shirika la Dada Yangu, Fatuma Ramadhan alisema kwa ushirikiamo na wadau mbalimbali wanalenga kuhakikisha jamii inapata elimu ya namna ya kukabiliana na ukatili huo wa kijinsia.
Fatuma Ramadhan pia alisema wanawake ndio waathiriwa wakuu wa dhuluma za kijinsia kupitia mitandao.
‘’Visa hivi vimekuwa vingi na ndio maana kuna haja ya kila mmoja kushiriki ipasavyo Katika kuhakikisha visa hivi vinadhibitiwa vilivyo na sio kuachia mashirika ya kijamii pekee’’ Alisema Ramadhan
Kwa upande wake Michael Baraka ambaye ni mhudumu wa bodaboda alisema watashirikiana katika kuripoti matukio hayo ili kudhibiti visa hivyo na kuitaka jamii kuondoa dhana kuwa vijana wa bodaboda wanahusika pakubwa katika utekelezaji wa dhuluma hizo.
‘’Kama wahudumu wa bodaboda tutashirikiana na kila mmoja kufanikisha hilo na pia kwa niaba ya wenzangu ningependa jamii iondoe dhana kuwa sisi tunahusika pakubwa katika visa vibaya’’ alisema Baraka.
Naye Shyleen Mumanyi wa shirika la Young Women Leadership Institute alisema katika kuhakikisha visa hivyo vinadhibitiwi watashirikiana pia na machifu na wazee wa nyumba kumi miongoni mwa viongozi wingine katika jamii.
Ni kauli ambayo iliungwa mkono na Abdulfah Nurein Mohamed huku akisema visa hivyo hasa kwa watoto huwa vinaongezeka zaidi wakati shule zimefungwa na kutoa wito kwa serikali ya kaunti ya Kilifi kuweka mikakati ifaayo katika kuimarisha usalama hasa katika fuo za habari na kusisitiza umuhimu wa wazee wa mtaa kujukumika vilivyo katika utendakazi wao.
Kwa kauli moja walikemea visa vya ukatili wa kijinsia pamoja na vile vya watu kupotea katika hali tatanishi na kutoa wito kwa serikali kuu kufanya uchunguzi wa visa hivyo kwa wakati na watuhumiwa wakabiliwe kisheria na pia kufanya kazi kwa karibu na mashirika yayototetea haki za wanawake.
Taarifa ya Janet Mumbi