Kilabu ya Arsenal yapata pigo, hii ni baada ya winga Bukayo Saka kutarajiwa kukosa mechi ya Arsenal dhidi ya Liverpool Jumapili pamoja na mechi za kufuzu Kombe la Dunia za England dhidi ya Andorra na Serbia mwezi ujao kutokana na jeraha.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aliumia msuli wa paja katika ushindi wa nyumbani wa Jumamosi dhidi ya Leeds United, na inakadiriwa atakuwa nje kwa muda wa hadi wiki nne.
Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard, pia yuko kwenye shaka ya kucheza mechi ya Anfield kutokana na jeraha la bega alilopata katika ushindi huo dhidi ya Leeds.
Odegaard alionekana kuumwa sana wakati alibadilishwa katika kipindi cha kwanza cha ushindi wa mabao 5-0, na inaelezwa aliondoka Uwanja wa Emirates akiwa na mkono katika kiwiko cha kushikilia bega.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa Norway hajathibitishwa kukosa kabisa mechi dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu, na kuna matumaini ndani ya Arsenal kwamba Odegaard mwenye umri wa miaka 26 na Saka hawatakuwa majeruhi wa muda mrefu.
Kuna afueni kubwa zaidi kuhusu Saka, ambaye alikosa miezi mitatu ya msimu uliopita kwa jeraha la msuli wa paja.
Arsenal msimu huu wana kikosi kipana zaidi cha washambuliaji baada ya kumsajili Viktor Gyokeres, Noni Madueke na Eberechi Eze majira ya kiangazi.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, pia ana Gabriel Martinelli, Leandro Trossard, Ethan Nwaneri na Max Dowman ili kuziba mapengo ya Saka na Odegaard.