Sports
Harambee Stars Hatua Moja Tu Kutinga Robo Fainali ya CHAN
Timu ya taifa ya soka Harambee Stars ipo hatua moja tu kuingia kwenye robo fainali ya michuano ya CHAN inayoendelea nchini Kenya, Uganda na Tanzania.
Hii inafuatia ushindi wa bao 1–0 walioupata dhidi ya mabingwa mara mbili Morocco, kwenye mchezo uliopigwa jana jioni katika Uwanja wa Kasarani.
Bao hilo pekee la mchezo liliwekwa wavuni dakika ya 41 kipindi cha kwanza na mshambulizi wa klabu ya Tusker FC, Ryan Wesley Ogam, mbele ya maelfu ya mashabiki walioufurika uwanjani kushuhudia pambano hilo.
Kocha Mkuu wa Harambee Stars Benni McCarthy alisema mechi hiyo haikuwa rahisi, lakini akawapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango cha juu mbele ya mashabiki wa nyumbani.
“Kwanza nawapongeza wachezaji wangu. Ilikuwa ni mechi ngumu dhidi ya Morocco, lakini vijana walijituma ipasavyo. Sina la kuwalaumu — wamepigana kama mashujaa. Shukrani pia kwa mashabiki wengi waliojitokeza; wametupa nguvu na kutusukuma kupata alama hizi tatu muhimu,” alisema kocha huyo.
Katika mchezo mwingine wa Kundi A, timu ya taifa ya Angola – Palancas Negras iliwashinda Chipolopolo ya Zambia kwa mabao 2–1 kwenye uwanja wa Nyayo.
Baada ya matokeo hayo, Harambee Stars wanasalia kileleni mwa kundi kwa alama 7, wakifuatwa na Angola wenye alama 4. Morocco na DR Congo wanashikilia nafasi ya tatu na nne mtawalia wakiwa na alama 3 kila mmoja, huku Zambia wakiburuza mkia bila alama.
Sports
Klabu ya Arsenal guu moja kuingia hatua ya Nusu fainali Klabu bingwa baada ya ushindi dhidi ya Sporting
Sports
Wakili George Kithi akabidhiwa rasmi Cheti cha uenyekiti wa bodi ya Michezo marufu kama Sports Arts and Social Development Fund (SASDF)
Waziri wa Wizara ya Masuala ya Vijana, Uchumi bunifu na Michezo, Salim Mvurya, ameshudia hafla rasmi ya kukabidhiwa uenyekiti wa Bodi ya Sports, Arts and Social Development Fund (SASDF) kutoka kwa Luteni Jenerali Mstaafu Jackson Tuwei kwenda kwa Mheshimiwa wakili George Kithi. Hafla hiyo ilifanyika, jijini Nairobi hii leo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Mvurya alimpongeza Luteni Jenerali (Mstaafu) Tuwei kwa uongozi wake wa mfano na kujitolea kwake katika kipindi chake cha utumishi. Alibainisha kuwa chini ya uongozi wake, bodi hio iliimarika na kuwa taasisi imara na yenye mwitikio zaidi katika kusaidia na kuendeleza vipaji vya Wakenya.
Aidha, Waziri alieleza imani yake kwa uongozi wa Mheshimiwa wakili George Kithi, akimhakikishia ushirikiano na msaada kamili kutoka kwa Wizara katika kutekeleza majukumu ya Bodi kwa kipindi chake cha miaka mitatu.
SASDF inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kulea na kukuza vipaji vya Kenya, pamoja na kuimarisha hadhi ya nchi kimataifa kupitia michezo na uchumi wa ubunifu. Kupitia uwezeshaji wa wanamichezo, wasanii na wadau wa utamaduni, mfuko huo unachangia pakubwa katika ukuaji wa sekta za michezo na ubunifu nchini.

