News
Mwili wa mtoto Keziah wasafirishwa Tarasaa kaunti ya Tanariver kwa mazishi
Jamaa na Marafiki walifika eneo la Mwezang’ombe kaunti ya Kilifi kuuaga mwili wa Kezia Matuki mwenye umri wa miaka saba na aliyekuwa mwanafunzi wa gredi ya pili ambaye mwili wake ulipatikana wiki chache zilizopita ukiwa umetupwa nje ya boma lao eneo hilo la Kwa Nzai, kabla ya kuusafirisha kwa ajili ya mazishi ambayo yameratibiwa kufanyika Jumamosi 16, Mei 2026 katika eneo la Tarasaa kaunti ya Tana River.
Waliotoa rambirambi zao kwa familia walilaani kitendo hicho, wakimtaja Keziah kama mtoto ambaye alikuwa akishirikiana na watoto wenzake vyema akiwa shuleni na hata nyumbani.
Vilevile, walisema kifo kimezima ndoto ya Kezia ambaye alikuwa mwanafunzi mwenye bidii shuleni.
“Kezia atakumbukwa na wengi kutokana na ucheshi wake na namna alivyokuwa akiiishi na watoto wenzake na hatujawahi kuskia ripoti zozote mbaya kumhusu kama za kuwachokoza wenzake” walisema waombolezaji

Mwili wa Keziah Matuki unaombolezwa na wengi kufuatia kifo chake tatanishi
Kwa upande wake naibu gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Chibule alilaani kitendo cha kuuawawa kwa Kezia na kutaka uchunguzi kuharakishwa ili haki ipatikame kwa familia na aliyehusika akabiliwe kisheria.
“Hili ni kisa cha kusikitisha Sana na asasi husika zinapaswa kuharakisha uchunguzi na aliyehusika awajibishwe kisheria ili iwe funzo kwa wengine” Alisema Chibule
Awali ripoti ya upasuaji wa mwili wa Keziah ulibaini kuwa aliuawa kwa kunyongwa.
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa alivunjwa shingo na kisha kunajisiwa.
Daktari mkuu wa hospitali ya rufaa ya Kilifi, Gilbert Angore, alisema sampuli zaidi zilipelekwa katika maabara ya serikali kwa uchunguzi wa kina.
Haya yanajiri huku mshukiwa wa mauaji hayo Dennis Otieno Oduor akiendelea kuzuiliwa rumande huko Shimo la Tewa kaunti ya Mombasa, uchunguzi unapoendelezwa.
Taarifa ya Janet Mumbi