News
Tume ya IEBC imepongeza zoezi la usajili wa wapiga kura wapya
Naibu Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Fahima Araphat amesema zoezi la usajili wa wapiga kura wapya linaendelea vyema licha ya changamoto mbalimbali.
Akizungumza katika ukumbi wa Kibaoni mjini Kilifi kaunti ya Kilifi kwenye hafla ya ushirikishaji wadau katika kutoa maoni kuhusu namna zoezi hilo linavyotekelezwa kaunti ya Kilifi, Araphat alisema kufikia Aprili 15 walikuwa wamesajili watu milioni 1.3.
Araphat pia alisema wakenya wanaendelea kujitokeza katika zoezi hilo na mikakati ifaayo imewekwa kuhakikisha wananchi wote wanasajiliwa kuwa wapiga kura ili washiriki uchaguzi mkuu ujao wa 2027 na kujitenga na madai kuwa IEBC inaegemei mrengo flani wa kisiasa.
‘’Sisi kama tume tutahakikisha kuna uwazi katika usajili huu na hata wakati wa kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu na tunaomba Wakenya wajitokeze kwa wingi kusajiliwa kuwa wapiga kura kabla ya kukamilika Aprili 28’’ Alisema Araphat
Wakati huohuo, Araphat akigusia suala la uratibu wa mipaka, alisema tume ya IEBC haiwezi kufanya uratibu huo kwa sasa ila mikakati inawekwa kuhakikisha unatekelezwa.
Naye meneja wa uchaguzi wa kaunti ya Kilifi Juma Musa Juma alitoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na IEBC ili fanikisha zoezi hilo la usajili wa wapiga kura wapya akitaja eneo bunge la Magarini kama ambalo linaongoza kwa usajili huo.
‘’ Tunahitaji ushirikiano wa kila mtu na idara ili zoezi ili litekelezwe kama lilivyoratibiwa’’ Alisema Musa
Kwa upande wake mwakilishi wa wadi ya Kibarani Moses Furaha Kea, alitoa wito kwa IEBC kuhakikisha idara inayohusika na usajili wa vitambulisho inaharakisha katika utoaji ili wananchi waweze kujisajili kuwa wapiga kura.
Nao wananchi waliohudhuria hafla hiyo waliitaka IEBC kufika mashinani ili kusajili idadi kubwa ya wapiga kura na kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kusajiliwa huku kamanda wa polisi eneo bunge la Kilifi Kaskazini Stanley Tunui na naibu kamishna wa Kilifi Kaskazini Samuel Mutisya wakisema idara ya usalama iko imara katika kuhakikisha usalama unaimarishwa vilivyo.
Taarifa ya Janet Mumbi