Uncategorized
Douglas Kanja, Mohammed Amin wakosa kufika mahakamani.
Siku kumi baada ya mwanablogu Ndiang’ui Kinyagia kutoweka, kesi ya kumtaka inspecta jenerali wa polisi Doglas Kanja kueleza alipo mwanablogu huyo iliendelea kusikilizwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi.
Inspecta jenerali wa polisi Douglas Kanja pamoja na mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI Mohammed Amin walikosa kufika katika mahakama kama ilivyo amriwa hapo awali.
Haya yanajiri huku maafisa wa DCI wakiongozwa na mkurugenzi wa DCI wakiiambia mahakama siku ya jumatatu 30 juni 2025 kwamba hawakumkamata mwanablogu huyo.
Kwa upande wake Jaji Chacha Mwita aliwataka wawili hao kuhakikisha wanaeleza alipo mwanablogu huyo.
“Hakuna vile mtu anaweza toweka ghafla na hajulikani alipo, hatutaki maneno mengi tunachotaka ni huyu mtu ako wapi mleteni mbele ya mahakama awe hai au mfu tunachotaka ni huyu mtu yupo wai?”,aliuliza jaji Chacha Mwita.
Viongozi mbalimbali akiwemo kinara wa chama cha PLP Martha Karua, mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili Owino maarufu Babu Owino miongoni mwa viongozi wengine walihudhuria kikao cha kesi hiyo huku Karua akisema kwamba, wawili hao wameonyesha utovu mkubwa na nidhamu kwa kukiuka amri ya mahakama.
Ikumbukwe kwamba mwanablogu Kinyagia alikamatwa tarehe 21 juni 2025 kwa kosa la uhalifu wa kimitandao ikiwa ni kuchapisha ratiba ya maandamano yaliyofanyika Jumatano tarehe 25 Juni 2025.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
Uncategorized
Mshukiwa wa mauaji kuzuiliwa rumande kwa siku 7
Mahakama ya Kilifi imeagiza kuzuiliwa rumande mshukiwa wa mauaji ya Ruth Ochieng’ mwenye umri wa miaka 60 kutoka kaunti ya Kisumu baada ya mshukiwa Evans Otieno kukamatwa katika Kanisa la Newlife Prayer Center lililoko eneo la Mavueni kaunti ya Kilifi.
Otieno alitiwa nguvuni na maafisa wa usalama alipokiri kwamba alitekeleza mauaji hayo mbele ya Mchungaji wa Kanisa hilo Ezekiel Odero, akitaka aombewe kama hatua moja wapo ya kutubu dhambi zake.
Hakimu wa Mahakama ya Kilifi Charles Obulutsa amesema Otieno atazuiliwa rumande kwa siku 7 ili kumuwezesha afisa wa polisi wa kituo cha polisi cha Seme mjini Kisumu anayechunguza kesi hiyo kufika Mahakamani.
Hakimu Obulutsa, ameeleza Mahakama kwamba wakati afisa huyo wa Polisi atakapofika katika Mahakama ya Kilifi atapewa idhini ya kumchukua mshukiwa ili afunguliwe mashtaka ya mauaji mjini Kisumu.
Awali Mahakama ilielezwa kwamba mwili wa mahehemu ulipatikana na kuthibitishwa kwamba alikuwa amenyongwa na uchunguzi zaidi ulikuwa unaendelea kabla ya mshukiwa kukamatwa katika maeneo ya Kanisa la Newlife Prayer Centre, eneo la Mavueni kaunti ya Kilifi.
Kesi hiyo itatajwa tena Februari 11 katika ili kuwakabidhi maafisa wa Polisi kutoka kaunti ya Kisumu mshtakiwa huyo.
Taarifa ya Teclar Yeri
Uncategorized
Wakenya wanaopata mshahara wa chini ya elfu 30 kuondolewa PAYE
Waziri wa Fedha nchini John Mbadi amesema serikali inalenga kuwaondolea ushuru wa PAYE wakenya wanaopata mshahara wa chini ya shilingi elfu 30 kwa mwezi huku wale wanaopata mshahara wa shilingi elfu 30 hadi laki tano wakitozwa ushuru wa asilimia 25.
Waziri Mbadi alisema hatua hiyo inalenga zaidi ya wakenya milioni 1.5 na hivi karibuni atawasilisha mswada bungeni ili pendekezo hilo liangaziwe na sheria ya ushuru ifanyiwe marekebisho kabla ya kupitishwa kwa mswada wa fedha wa mwaka wa 2026.
Waziri Mbali aliyasema hayo wakati wa kikao cha kukusanya maoni ya umma katika kaunti ya Meru ambapo alikuwa amefanya kikao cha mazungumzo na Rais William Ruto na kuafikiana kuhusu pendekezo hilo.
Waziri huyo wa fedha nchini aliongeza kwamba mswada huo pia utajumuisha pendekezo la kupunguza ushuru wa PAYE kwa asilimia 5 kwa wakenya wanaopokea mshahara wa kati ya shilingi elfu 32,050 kwa mwezi hadi shilingi laki tano, akisema punguzo hilo la asilimia 5 litasaidia wakenya kumudu gharama ya maisha.
“Tumekubaliana na Rais kwamba wananchi wenye kipato cha chini wanapaswa kupata nafuu kwenye mishahra yao kwani idadi kubwa ya wananchi wanapitia hali ngumu ya maisha na hatua hii itasaidia wakenya wengi kuwa na pesa mfukoni. Sidhani kama kuna mbunge yeyote atapinga pendekezo hilo”, alisema Mbadi.
Waziri huyo wa fedha alishikilia kwamba hatua hiyo inalenga kupunguza mzingo wa ushuru kwa wakenya wa kipato cha chini na cha kati na kuwasaidia kujikimu katika kipindi hiki cha gharama ya juu ya maisha.
Kwa sasa kikomo cha ushuru wa PAYE kinaathiri wakenya wengi wenye kupokea mshahara wa kuanzia shilingi elfu 24, akisema wataalamu wamebaini kwamba kupunguzwa kwa ushuru kutachangia matumizi ya nyumbani kuwa ya usawa na kusaidia kuimarisha uchumi unaokabiliwa na mahitaji duni.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

