News
Ethekon: Uchaguzi mkuu utakuwa huru, haki na uwazi
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imeanza rasmi zoezi la kuwasajili wapiga kura wapya kote nchini, huku ikilenga kuwasajili wapiga kura milioni 6.2, kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Erastus Ethekon aliwahakikishia wakenya kwamba makamishna wa tume hiyo watahakikisha uchuguzi mkuu ujao unakuwa huru, haki na uwazi.
Akizungumza katika kaunti ya Kwale wakati wa kuzindua wa zoezi la usajili wa wakipiga kura kote nchini, Ethekon alisema serikali imewekeza raslimali za kutosha za kufanikisha zoezi hilo.
“Nataka kuwahakikishia wakenya kwamba tumejipanga kama IEBC na tuko na raslimali za kutosha kuhakikisha zoezi la usajili wa wapiga kura linaendeshwa vyema na uchaguzi mkuu utakuwa huru, haki na wazi ili kuhakikisha wakenya wanatekeleza jukumu lao la kidemokrasia na hatua hiyo tutafikia idadi ya wapiga kura zaidi ya milioni 27”, alisema Ethekon.
Naye Naibu Mwenyekiti wa IEBC Fahima Araphat alisema tayari maafisa wapya wa IEBC elfu 12 wameajiriwa kuhakikisha zoezi hilo liendeshwa vyema ili kusajili idadi kubwa ya wapiga kura
“Sisi tunafanya kazi yetu bila kuegemea upande wowote wa kisiasa na tuko tayari kuhakikisha anashinda uchaguzi anatangazwa mshindi kwa haki, na kama tuko na makarani elfu 12 na wote wasajili wapiga kura wapya elfu 10 kila moja tutakuwa na idadi kubwa ya wapiga kura, sasa hiyo ndio tunalenga kupata”, alisema Fahima.
Kwa upande wake Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani, aliipongeza tume hiyo kwa zoezi hilo endelevu la wapiga kura, akisema ni hatua ya kipekee kwa jamii ambazo zimekosa fursa ya kujisajili kama wapiga kura.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
IEBC yasema idadi ya wanaojisajili ni ndogo mno
Zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura kote nchini limeng’oa nanga huku maafisa wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wakilenga idadi kubwa ya vijana katika zoezi hilo.
Katika kaunti ya Kilifi eneo bunge la Kilifi Kazkazini, zoezi hilo limefanyika katika vituo vinne tofauti huku idadi ndogo ya wapiga kura ikishuhudiwa licha ya vuguvugu la TUKO KADI kuanzishwa na vijana ili kuwajisajili wapiga kura.
Akizungumza na Wanahabari wakati wa zoezi hilo, Naibu Afisa wa usajili wa wapiga kura katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini Abdul Mohammed aliwarai vijana kujitokeza kwa wingi na kujisajili.
Mohammed pia aliwarai vijana kukoma kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa manufaa yao binafsi, akipongeza vuguvugu lilionzishwa na vijana la TUKO KADI kama njia moja ya kuwahamasisha vijana kujisajili kama wapiga kura.
“Tumeanza zoezi hili na tunawahimiza vijana wajitokeze kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kutumia nafasi hiyo kuchagua viongozi wanawataka na wala wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa”, alisema Mohammed.
Kwa upande wao baadhi ya vijana waliojisajili waliwarai vijana wenzao kujitokeza kwa wingi na kushiriki zoezi hilo ili kuchagua viongozi wanaohisi wataleta maendeleo sawa na kubuni nafasi za ajira.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Chuo cha kiufundi cha Godoma taabani
Ripoti iliyotolewa na Wizara ya elimu nchini kuhusu vyuo vya kiufundi vya TVETs ilibaini kwamba idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo bado iko chini mno.
Hii ni baada ya vijana wanaofaa kujiunga na vyuo hivyo kusalia nyumbani licha ya serikali kutumia raslimali za umma kujenga taasisi hizo muhimu hadi mashinani.
Chuo cha kiufundi cha Godoma kilichoko eneo la Vitengeni katika eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi huenda kikawa kati ya vyuo vitakavyofungwa kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi.
Kati ya wanafunzi 500 katika chuo hicho, asilimia 80 ya wanafunzi hao ni wale waliotumwa na Shirika la huduma kwa vijana wa taifa NYS huku asilimia 20 wakiwa wanafunzi kutoka eneo bunge la Ganze na sehemu zengine za nchi, hali inayoibua wasiwasi.
Hatua hii iliwalazimu wadau wa sekta ya elimu kutoka serikali kuu, maafisa wa usalama, wakaazi pamoja na machifu kwa ushirikiano na usimamizi wa chuo hicho kufanya mkutano wa kuangazia jinsi watakavyosajili wanafunzi.
Katika mkutano uliyoandaliwa katika chuo hicho cha kiufundi cha Godoma, ulibaini sababu zilizochangia wanafunzi kuondoka chuoni na wengine kusalia nyumbani, mojawapo ikiwa ongezeko la karo kinyume na taasisi zengine.
Chuo hicho ambacho awali kilikuwa na idadi ya wanafunzi zaidi ya elfu moja, sasa idadi hiyo imeonekana kushuka hadi wanafunzi 500 na kusababisha hofu ya hatima ya chuo hicho hali ambayo wadau wa elimu waliahidi kuandaa mikakati ya kuzuru mashinani kuzungumza na vijana ili kujiunga na chuo hicho.

Wanafunzi wa chuo cha kifundi cha Godoma eneo la Vitengeni, eneo bunge la Ganze
Maafisa tawala kwa ushirikiano na wale wa chuo hicho wakiongozwa na Afisa wa kitengo cha mauzo katika ofisi ya Katibu wa vyuo vya kiufundi Tvets, Benson Mwakima wameitikia wito wa kuzuru mashinani na kuwahamaisha vijana.
Zoezi hilo limepangwa kuanza rasmi Aprili 9 mwaka huu, ili kueleza vijana jinsi ya kutambua umuhimu wa mafunzo ya vyuo vya Tvets pamoja na kuwaeleza jinsi ya kupata mikopo ya karo kupitia bodi ya kitaifa ya elimu kuhusu mikopo, HELB.
“Tutazuru mashinani kuanza tarehe 9 mwezi Aprili na kuzungumza na wazazi na vijana wetu kuwaeleza kuhusu mafunzo ya vyuo vya kiufundi ili wajiunge na shule na suala la karo pia tutawaeleza kwa sababu hapa shuleni kwetu tunahitaji wanafunzi”, alisema Afisa wa usajali wa wanafunzi katika chuo hicho, Eric Mutai.
Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho Emmanuel Masha, alilalamikia hatua ya Mwalimu mkuu wa taasisi hiyo Sebastian Shikoli ya kutohudhuria mkutano huo, akisema atafanya kikao naye ili kuangizia suala hilo ikiwemo ongezeko la karo lililoibuliwa na wazazi kama changamoto kuu.
“Ni jambo la kushangaza kwamba Mwalimu mkuu hayuko kwa mkutano huu na hapa kuna masuala muhimu ambayo yanapaswa kuzungumziwa hasa suala hili la karo lakini tunajua kwamba alishikika kwa majukumu mengine, nitaongea naye, najua atakuwa ofisini wiki ijayo”, alisema Masha.
Afisa anayesimamia kituo cha polisi cha Vitengeni Mohammed Ali alisema hatua ya kuzuru mashinani na kuwahamasisha vijana waliosalia nyumbani kujiunga na vyuo vya Tvets itapunguza visa vya uhalifu mashinani.
“Tusaidiane hapa ili tufanye chuo chetu kiwe na wanafunzi na hatua hii itatusaidia sana sisi kama maafisa wa usalama kuhakikisha visa vya uhalifu vinapungua kwa sababu hawa vijana wakikaa mtaani watajihusisha na mambo maovu”, alieleza Ali.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

