International News
Trump asema Marekani itasitisha vita dhidi ya Iran
Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani itaondoka Iran hivi karibuni na hatua za kijeshi za nchi hiyo zitakomeshwa ndani ya wiki mbili au tatu zijazo.
Rais Trump alisema Marekani imefikia malengo iliyojiwekea kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mwezi uliyopita kwa ushirikiano na Israel.
Aidha aliongeza kuwa lengo la kuizuia Iran kuwa na uwezo wa kuunda silaha za nyuklia limefikiwa na sasa Marekani inamaliza kazi.
Trump pia aliema Marekani sasa inatawala anga za Iran na pia imepata mabadiliko ya utawala kufuatia mauaji ya viongozi wakuu wa kisiasa na kijeshi.
Aliwataja viongozi hao wapya mjini Tehran kama walio na misimamo mikali na waadilifu zaidi, ikilinganishwa na watangulizi wao.
Trump pia alisema viongozi wa Iran wanaomba kufanya makubaliano na Marekani ili kumaliza vita, madai ambayo hapo awali yalipingwa na Iran na kuongeza kwamba vita vinaweza kumalizika bila makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Kuhusu athari za vita hasa kupanda kwa bei ya mafuta, rais Trump alisema bei itashuka mara tu Marekani itakapomaliza hatua zake za kijeshi.
International News
Vita dhidi ya Al-Shabab vya shika kasi Somalia
Operesheni kali ya kijeshi inayoendelea nchini Somalia ambapo zaidi ya wanamgambo 33 wa kundi la Alshabab wameuawa katika eneo la Shabelle nyanda za chini za Jubaland.
Ufanisi wa operasheni hii ya hivi punde ni muendelezo wa oparesheni iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Aprili 24 katika eneo hilo la Juba ambapo Wanamgambo 27 wa AlShabab waliuawa.
Hii ina maana kwamba Jeshi la Somali limefanikiwa kuvunja maficho muhimu ya kundi hilo, ambalo kufikia sasa ya Wanamgambo 60 wameuawa
Kwa mujibu wa vianzo vya habari hususan kutoka kwa maafisa wa usalama, operesheni hiyo inafanyika kufuatia taarifa za kijasusi kuhusu maficho ya wanamgambo hao waliokuwa wakipanga mashambulizi dhidi ya vituo muhimu na taasisi za serikali.
Wanajeshi hao walivamia ngome za magaidi hao kwa ustadi mkubwa, wakifanikiwa kudhibiti eneo hilo baada ya mapambano makali yaliyochukua muda wa saa kadhaa.
Maafisa wamesema kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha usalama na kuangamiza kabisa mtandao wa Al-Shabaab ambao kwa muda mrefu umekuwa ukihatarisha amani katika maeneo mbalimbali ya Somalia na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Wananchi wa eneo la Jubbaland wameelezea matumaini mapya kufuatia operesheni hiyo, wakisema kuwa hatua hiyo inaleta nuru ya kurejea kwa utulivu na maendeleo baada ya miaka ya hofu na mashambulizi ya mara kwa mara nchini.
Serikali imeapa kuendeleza msako dhidi ya wanamgambo hao hadi pale watakapokomesha kabisa vitisho vya mashambulio , huku ikiwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti ugaidi.
Taarifa ya Billy Mongo
International News
Kumbukumbu za muaji ya kimbari Rwanda
Ni miaka 32 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
Leo, tarehe saba Aprili, raia wa Rwanda pamoja na dunia kwa ujumla wanaungana kukumbuka kuanza kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo zaidi ya watu laki nane, wengi wao wakiwa jamii ya Watutsi, waliuawa ndani ya kipindi cha siku mia moja.
Tarehe hii ni ya kihistoria kwa taifa hilo ambalo miaka 32 iliyopita lilikumbwa na moja ya matukio ya kikatili zaidi katika historia ya mwanadamu.
Mauaji hayo yalichochewa na kuuawa kwa aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana, tukio lililosababisha kuzuka kwa vurugu kote nchini.
Kilichofuatia ni mashambulizi ya kimbari kati ya Wahutu na Watutsi, ambapo zaidi ya watu milioni moja wanaripotiwa kupoteza maisha katika muda wa siku mia moja.
Wanawake, wanaume na watoto walilengwa katika mashambulizi hayo yaliyopangwa, jamii zikivunjika na dunia ikishuhudia tukio hilo kwa muda bila kuchukua hatua za haraka kuzuia maafa hayo.
Katika kuadhimisha siku hii, inayojulikana kama KWIBUKA, yenye maana ya “tunakumbuka,” bendera nchini Rwanda zinapepea nusu mlingoti, huku Rais Paul Kagame akitarajiwa kuwasha mwenge wa kumbukumbu katika makavazi ya Kigali.
Hata hivyo, licha ya historia hiyo ya maumivu, Rwanda imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ikijijenga upya kutoka jamii iliyogawanyika hadi kuwa taifa lenye umoja, likishuhudia maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na juhudi za maridhiano na haki kwa wahanga.
Leo hii, Rwanda inasimama kama mfano kwa mataifa mengine aduniani, huku wito wa kuhakikisha mauaji ya kimbari hayajirudii tena ukiendelea kusisitizwa.
Taarifa ya Hamis Kombe

