Business
Kanisa Katoliki lahimiza umuhimu wa Kilimo
Kasisi wa Kanisa Katoliki jimbo la Malindi Misheni ya Mere kaunti ya Kilifi, Blaise Kamau Andrew ametoa wito kwa wenyeji wa Pwani kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa ili kupata chakula cha kutosha na kilicho bora.
Akizungumza katika eneo la Kwa Ndomo eneo bunge la Malindi, Kasisi Kamau aliesema ikiwa Wapwani watatia juhudi katika sekta ya kilimo huenda kukawa na mavuno mengi na chakula cha kutosha ili kudhibiti njaa wakati wa kiangazi.
Kasisi Kamau pia aliwashinikiza kuchimba visima vingi vya maji ili panapokosekana mvua kuwe na maji ya kutosha ya kuendeleza kilimo nyunyizi.
“Chibeni visima ili usiwe mkulima wa kungojea tu mvua ya mwenyeji Mungu.Tufanyeni bidi wengi wenu wana Ng’ombe, wengi wenu wana mbuzi uza Ng’ombe mbili, chimba kisima maji hayako mbali sana ili mvua ikikatika bado mnaendeleza kilimo nyunyizi’’, alisema Kasisi Kamau.
Ni kauli ambayo imeungwa mkono na msimamizi wa kitengo cha chakula na Kilimo katika benki ya Equity tawi la Nairobi, George Macharia ambaye alisema ili kuimarisha uchumi wa Kenya ni lazima Wapwani na wakenya kwa jumla wakumbatie kilimo cha kisasa kupitia mfumo wa teknolojia.
“Ili tuweze kupanua uchumi ni lazima tuwekeze katika kilimo na tuhakikishe tunatumia kilimo cha kisasa cha kiteknolojia’’, Macharia aliwasihi Wakulima.
Taarifa ya Janet Mumbi
Business
Bei za mafuta kuongezeka katikati ya mwezi aprili
Kenya sasa inakabiliwa na hatari ya kupanda kwa bei za mafuta, huku mgogoro unaoendelea mashariki ya Kati ukianza kuathiri bei nchini.
Serikali sasa imeonya kuwa kufikia katikati ya mwezi Aprili, bei za mafuta huenda zikapanda ikionya kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwa sasa haliwezi kuepukika kufuatia kupanda kwa bei za mafuta kimataifa.
Waziri wa hazina kuu ya kitaifa John Mbadi aliwahakikishia wakenya kuwa hakuna cha kuhofia kwani wameweka mikakati kupunguza athari zake.
Ili kupunguza athari za bei za mafuta kuongezeka, serikali ilisema itatumia shilingi bilioni 17 kutoka mfuko wa ada ya uwekezaji wa mafuta kusaidia kudhibiti bei kwa mda wa miezi 3 ijayo.
Kwa sasa serikali inasema kuna akiba ya kutosha ya mafuta na shehena zaidi zinatarajiwa nchini hivi karibuni.
Taarifa ya Joseph Jira
Business
KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa
Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.
Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

