News
Kaunti ya Lamu yaandaa jukwaa la kuangamiza ukame
Kaunti ya Lamu imeandaa Awamu ya Pili ya mkutano wa ngazi ya juu kwa ajili ya kuangazia mikakati ya kuangamiza ukame ambayo ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha ustahimilivu wa muda mrefu na usimamizi wa kukabiliana na majanga katika kaunti nzima.
Mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Ardhi, maji na Nishati katika kaunti hiyo Tashrifa Abubakar, pamoja na wadau wa Mamlaka ya kitaifa ya kukabiliana na Ukame (NDMA) pia uliwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya serikali na washirika wa maendeleo.
Washiriki walielekezwa kuhusu vipengele muhimu vya mfumo wa awamu ya Pili ya kuangamiza ukame, unaolenga kuhamia kutoka hatua za dharura za kukabiliana na ukame kuelekea mifumo endelevu ya muda mrefu.
Washiriki wamethibitisha dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano chini ya muundo wa jukwaa la uratibu katika ngazi ya kaunti- CSG, wakitambua kuwa ni jukwaa muhimu la kupanga kwa pamoja, kufanya maamuzi, na kutekeleza mipango.
Mkutano huo pia ulitumika kama jukwaa la kusherehekea utambuzi wa kimataifa wa hivi karibuni wa Kaunti ya Lamu kupitia Tuzo za Kimataifa za Water Transversality, ambapo Mpango wa Uondoaji Chumvi na Usimamizi wa Maji wa Kiunga ulitunukiwa kama Mradi Bora wa Athari kwa Jamii (2026).

Viongozi wa kaunti ya Lamu pamoja na Mamlaka ya kukabiliana na ukame na washkadau mbalimbali wanafanya kikao cha kuangazia mikakati ya kudhibiti ukame
Mradi wa Kiunga ni mfano bora wa ustahimilivu jumuishi unaoongozwa na jamii.
Awali ulianzishwa kufuatia uhaba mkubwa wa maji uliosababisha migogoro ya rasilimali, suala ambalo liliwasilishwa kwa jukwaa la uratibu katika ngazi ya kaunti kwa majadiliano.
Viongozi wamesisitiza kuwa mafanikio ya mradi wa Kiunga na utambuzi wake wa kimataifa yalitokana moja kwa moja na uratibu madhubuti chini ya mfumo wa Jukwaa hilo, ukiungwa mkono na Mamlaka ya Kitaifa ya kukabiliana na Ukame-NDMA.
Kaunti hiyo imethibitisha nafasi yake kama mfano bora wa jinsi mbinu jumuishi za sekta mbalimbali zinavyoweza kushughulikia kwa ufanisi changamoto za ukame, migogoro, na mabadiliko ya tabianchi.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Waziri Wandayi asema hatajiuzulu
Waziri wa Kawi nchini Opiyo Wandayi ameweka wazi kwamba hatajiuzulu licha ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na mashirika ya kijamii, kumtaka ajiuzulu.
Wandayi alisema haoni sababu za kuchukua uamuzi huo kwani hausiki kivyovyote na sakata ya uagizaji wa mafuta ghushi, akisema uchunguzi unaendelea kuhusu suala hilo.
Akijubu maswali yalioulizwa na wabunge mbele ya kamati ya Kawi katika bunge la kitaifa, inayoongozwa na David Gikaria, Waziri hiyo alisema hadi kufikia sasa hajajua kiini kilichowashinikiza maafisa watatu katika wizara yake waliohusisha na sakata hiyo kujiuzulu.
Wandayi alithibitisha kwamba Idara ya Mafuta chini ya Wizara ya Kawi nchini iliomba msamaha wa vigezo fulani kutoka kwa Shirika la ukadiriaji wa bidhaa nchini (KEBS) kupitia barua za tarehe 26 na 27 Machi 2026. Msamaha huo ulitolewa baadaye na Wizara ya Biashara na Viwanda nchini inayoongozwa na Lee Kinyanjui kuridhinia msamaha huo tarehe 28 Machi 2026.
Aidha alifichua kwamba Kamati ya uratibu wa Meli (VAC) ilibaini mnamo tarehe 18 Machi 2026 kuwa meli iliyokuwa imepangwa ilikuwa imepakia mizigo katika bandari ya Jebel Ali lakini haikuweza kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, hali iliyozua hofu ya uwezekano wa pengo la usambazaji wa mafuta.
Ilibainika kwamba kauli ya mashirika mbalimbali iliyopendekeza mzigo wa dharura uliwasilishwa kwa Katibu wa Wizxara ya Kawi na mafuta nchini Mohammed Liban kuidhinisha.
Waziri Wandayi hata hivyo alipoulizwa ni wapi hasa usambazaji wa mafuta ulikwama, aliwaelekeza wabunge kwa taratibu za ndani za Kampuni ya usambazaji mafuta (KPC), akisema kuwa kampuni hiyo ilipokea ripoti ya bandari ya kupakia mizigo tarehe 27 Machi ili kuhakikisha inazingatia viwango vinavyohitajika.
Wakati huo huo alidokeza kwamba hakuna na ufahamu kwamba sakata hiyo ilikuwa kinyume na mpango wa uagizaji wa mafuta wa serikali kwa serikali yani G to G, akisema hatua hiyo ndio iliyopelekea kuanzishwa kwa ucnguzi na maafisa wa DCI.
News
ODM yatishia kujiondoa katika serikali jumuishi
Huenda mpango wa serikali jumuishi uliobuniwa na rais William Ruto na aliyekuwa Kinara wa chama cha ODM hayati Raila Odinga ukavunjika iwapo masuala ibuka yaliyowasilishwa na Chama cha ODM yatakosa kutimizwa.
Chama hicho kimekosoa jinsi baadhi ya wafuasi wa chama cha UDA kujitenga na mwenzao wa ODM licha ya kuwepo na mpango wa serikali jumuishi pamoja na kukosoa kutishiwa kwa baadhi ya viongozi wa ODM kujiondoa na chama hicho ili wajiunge na UDA.
Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kitaifa Junet Mohammed alisema kuna njama ya kusambaratishwa kwa ushawishi wa chama cha ODM katika maeneo ya Nyanza na Pwani kwani kuna taarifa kwamba baadhi vya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakishurutishwa na maafisa wa Ikulu ya rais.
Junet ambaye pia ni mbunge wa Suna Mashariki, alisisitiza kwamba ODM kujiunga na UDA haikuwa na makusudi bali serikali ilihitaji msaada wa viongozi wa chama hicho ili kulinusuru taifa kwani lilikuwa linaelekea mahali pabaya.
“Hatuko kwa serikali jumuishi kimakosa ama kimakusudi wala kwa mualiko bali tuliingia katika serikali jumuishi kutokana na serikali ya rais Ruto kutaka msaada watu ili kulinusuru taifa lakini kama uongozi wa UDA unaona kumetengeza misingi na umaarufu mashinani tunaweza kuwaacha watengeze serikali yao mwaka 2027”, alisema Junet.
Kiongozi huyo ambaye pia ni Mwanachama wa Kamati kuu ya chama hicho alisema wataisha mkutano wa dharura wa Kamati kuu ili kuangazia suala hilo kwani mvutano huo huenda ukazidi kushamiri iwapo hakutakuwa na mikakati mwafaka.
Katika siku za hivi majuzi katika siasa za mashinani, chama cha UDA kimeonekana kikiendeleza siasa za kuimarisha chama hicho pamoja na kusajili wanachama wapya ili kujienga umaarufu zaidi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Viongozi wa UDA walionekana kutangaza hadharani kwamba hakutakuwa na mpango wa kusimamisha mgombea mmoja katika eneo kwenye serikali jumuishi yaani Zoning bali kila kiongozi akijipange kisiasa na kupambana katika nyadhfa anayoelenga kushikilia wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

