News
KEMNAC, yaunga mkono taifa la Tanzania kutoruhusu Wanaharakati wa Kenya
Baraza kuu la mashauri ya Waislamu nchini KEMNAC limeunga mkono taifa la Tanzania kwa kutoruhusu Wanaharakati wa kijamii na baadhi ya viongozi kutoka Kenya kuingilia siasa za taifa hilo.
Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Juma Ngao, alisema Tanzania kuna amani na utulivu mkubwa ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika mashariki.
Sheikh Ngao, aliwataka vijana wanaotengeneza maudhui na semi za kutisha na kumkejeli Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kukoma mara moja, akisisitiza kuwa ni kumkosea heshima na kumdhalilisha kiongozi huyo bila sababu za msingi.
Sheikh Ngao alisema taifa la Kenya limejaa ukabila na chuki za kisiasa tofauti na na taifa la Tanzania ambalo linajulikana kuwa taifa lenya amani na uzalendo huku akiwataka wakenya kuimarisha umoja na mshikamano kabla ya kuenda kutafutia amani nchi zengine.
“Tanzania tangu ipate uhuru wake, jeshi lake halijathubutu kupindua nchi hapa waliothubutu, hakujaandamanwa kuvamia bunge na kulichoma hapa ilifanyika, hakujapiganwa mpaka kukapatikana Waziri mkuu wa nchini kule kulipatikana Waziri mkuu kisheria, kwa hivyo Kenya huweze kuwafundisha watu wa Tanzania mambo ya Amani”, alisema Sheikh Ngao.
Kwa upande wake, Abubakar Amin Al’alawi, ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo, aliwataka viongozi wa kidini, kijamii, na wazazi kuwaelimisha vijana na watoto wao kuhusu maadili mema ili kuepuka chuki miongoni mwa mataifa haya mawili.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

