International News
Mojtaba Khamenei kutangwa kiongozi mpya wa Iran
Iran inatarajiwa kumtangaza kiongozi mkuu mpya atakayechukua nafasi ya Ayatollah Ali Khamenei aliyeuawa wiki moja iliyopita kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel.
Mmoja wa wajumbe wa Baraza la wataalam alidokeza kwamba kuna uwezekano mkubwa mtoto wa Khamenei, Mojtaba Khamenei mwenye umri wa miaka 56, akachaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi alisema viongozi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ndio watakaomchagua kiongozi wao na wala sio rais wa Marekani Donald Trump kama alivyodai.
Wakati vita vikiingia siku ya tisa, mashambulizi yalishuhudiwa kila upande.
Israel ilishambulia maghala na vituo vya kuhifadhi mafuta mjini Tehran huku Iran nayo ikivurumisha makombora na droni kuelekea Israel na katika nchi zingine za Ghuba.
Watu sita waliripotiwa kujeruhiwa huko Israel huku wanajeshi wawili wa Israel wakiuwa kusini mwa Lebanon.
Jeshi la walinzi wa mapinduzi wa Iran limesema lina uwezo wa kuendeleza mapigano hadi miezi sita na limeonya kuwa awamu inayofuata ya mashambulizi inaweza kuhusisha makombora ya kisasa ambayo hayajawahi kutumika katika vita.
Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump, alikataa kuondoa uwezekano wa kutuma wanajeshi wa ardhini nchini Iran, hatua ambayo inaweza kuongeza hatari ya vita katika eneo hilo.
Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo katika ibada ya Misa siku ya Jumapili tarehe 8 mwezi Machi, 2026 alihimiza kukomeshwa kwa vurugu na kuanzisha juhudi mpya ili kuendeleza mchakato wa mazungumzo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
International News
Vita vya Iran vyasambaratisha biashara za kimataifa.
Vita vya Iran vinaweza kuisha hivi karibuni au kuendelea kwa miezi kadhaa licha ya tamko la rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mpango ya kumaliza vita hivyo.
Iwapo vita hivyo vitakomeshwa basi Hormuz itakapofunguliwa tena ilhali mtihani halisi utakuwa ni vipi minyororo ya usambazaji wa nishati, mbolea na bidhaa nyingine itaweza kurejea haraka.
Wakati wale wenye matumaini wakianza kuhisi kwamba vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilikuwa karibu kumalizika, mgogoro huo wa mwezi mzima unachukua mwelekeo mwingine tena.
Rais wa Marekani Donald Trump alionya Tehran kwamba hakutakuwa na kurudi nyuma kuhusu mashambulizi yaliyoongozwa ya Marekani, kinyume na kauli yake kwamba hivi karibuni Marekani itaondoka Iran na hatua za kijeshi za nchi hiyo zitakomeshwa ndani ya wiki mbili au tatu zijazo.
Iran, kwa upande wake, inaruhusu idadi ndogo ya meli kupita katika Mlango wa Hormuz, huku ikikanusha kuwa mazungumzo yoyote ya kusitisha vita yanaendelea.
Wataalamu wengi wanakubaliana juu ya jambo moja muhimu: kadiri mzozo huu unavyoendelea kwa muda mrefu, ndivyo athari zake zitakavyokuwa mbaya zaidi kwa usambazaji wa nishati duniani, mfumuko wa bei na uthabiti wa uchumi.
Benki ya hifadhi ya Shirikisho ya Dallas, ambayo ni sehemu ya mfumo wa benki kuu ya Marekani, ilitabiri mapema mwezi huu kwamba kufungwa kwa mlango huo kwa miezi mitatu au zaidi kungesababisha ukuaji wa pato la taifa la dunia kupungua kwa asilimia 2.9 kwa mwaka katika robo ya pili ya mwaka.
International News
Trump asema Marekani itasitisha vita dhidi ya Iran
Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani itaondoka Iran hivi karibuni na hatua za kijeshi za nchi hiyo zitakomeshwa ndani ya wiki mbili au tatu zijazo.
Rais Trump alisema Marekani imefikia malengo iliyojiwekea kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mwezi uliyopita kwa ushirikiano na Israel.
Aidha aliongeza kuwa lengo la kuizuia Iran kuwa na uwezo wa kuunda silaha za nyuklia limefikiwa na sasa Marekani inamaliza kazi.
Trump pia aliema Marekani sasa inatawala anga za Iran na pia imepata mabadiliko ya utawala kufuatia mauaji ya viongozi wakuu wa kisiasa na kijeshi.
Aliwataja viongozi hao wapya mjini Tehran kama walio na misimamo mikali na waadilifu zaidi, ikilinganishwa na watangulizi wao.
Trump pia alisema viongozi wa Iran wanaomba kufanya makubaliano na Marekani ili kumaliza vita, madai ambayo hapo awali yalipingwa na Iran na kuongeza kwamba vita vinaweza kumalizika bila makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Kuhusu athari za vita hasa kupanda kwa bei ya mafuta, rais Trump alisema bei itashuka mara tu Marekani itakapomaliza hatua zake za kijeshi.

