News
Mwinyi, awaonya wakenya dhidi ya siasa za migawanyiko
Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Mombasa wakiongozwa na mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi wamewakosa wananchi pamoja na viongozi dhidi ya kuendeleza siasa za migawanyiko, taifa linapojiandaa kwa kipute cha uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2027.
Mwinyi alisema taifa la Kenya linahitaji maendeleo na sio siasa zinazosababisha migawanyiko kwa Wakenya kwa misingi ya vyama vya kisiasa na ukabila.
Mwinyi pia aliwakosa wale ambao wanawadhalilisha wanawake kutokana na misimamo yao ya kisiasa.
“Huyu Zamzam anaheshimiwa kitaifa, wewe mtu wa Mombasa kwa nini umtukane. Kwa hivyo wenye siasa hizo wakome’’Alisema Mwinyi.
Naye Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir aliwahimiza viongozi kutoka mirengo mbalimbali ya kisisa kushirikiana ili kuwe na amani katika taifa hili la Kenya kauli ambazo zimeungwa mkono na baadhi ya wawakilishi wa wadi katika kaunti hiyo.
“Mimi nawaomba tuungane kama viongozi na tuweka tofauti zetu za kisiasa kando, 2027 ikifika mwenyezi Mungu atatujalia yule ambaye atakuwa gavana maana uongozi unatoka kwa Mungu, binadamu ni sababu’’, alisema Nassir.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

