Sports
PSG Yatwaa UEFA Super Cup Kwa Mara Ya Kwanza Baada ya Kuibwaga Spurs kwa Penalti
Mabingwa wa Ulaya kilabu ya Paris Saint-Germain (PSG) walianza msimu mpya kwa kutwaa tena kombe Jumatano usiku baada ya kuwashinda Tottenham Hotspur kwa penalti 4-3 katika UEFA Super Cup, kufuatia kurejea kwa kishindo dakika za mwisho na kulazimisha sare ya 2-2.
Kilabu ya Tottenham HotSpurs walionekana kuwa karibu na taji hilo katika mechi yao ya kwanza rasmi chini ya kocha mpya Thomas Frank, baada ya kuongoza 2-0 muda mfupi baada ya kipindi cha pili kuanza katika uwanja wa Stadio Friuli mjini Udine, Italia.
Beki wa Uholanzi Micky van de Ven aliwapa mabingwa hao wa Europa League wa msimu uliopita uongozi dakika ya 39 kabla ya beki mwingine Cristian Romero kuongeza la pili dakika ya 48. Hata hivyo, PSG waliokolewa na wachezaji wawili wa akiba, ambapo Lee Kang-in alifunga dakika ya 85 na Goncalo Ramos kusawazisha kwa kichwa dakika ya 94.
Hali hiyo ilisababisha mchuano kuamuliwa kwa penalti, ambapo PSG walianza vibaya baada ya Vitinha kupiga nje penalti ya kwanza.
Kipa mpya wa PSG Lucas Chevalier alidaka penalti ya Van de Ven huku Mathys Tel akikosa shabaha, jambo lililomruhusu Nuno Mendes kufunga penalti ya ushindi kwa PSG.
Dominic Solanke, Rodrigo Bentancur na Pedro Porro walifunga penalti zao kwa Spurs, bila mafanikio. Kwa upande wa PSG, Ramos, Ousmane Dembele na Lee walifunga kabla ya Mendes kupiga ya mwisho na kuihakikishia PSG ushindi.
Ni mara ya kwanza kwa PSG, na hata klabu yoyote ya Ufaransa, kutwaa Super Cup, huku sasa wakifikisha mataji matano mwaka huu wa 2025.