Business
Viongozi wa Mombasa Waisihi Serikali Kuu Kuwekeza Zaidi Katika Uchumi wa Samawati
Viongozi wa kaunti ya Mombasa wameitaka serikali kuu kuongeza uwekezaji katika sekta ya uchumi wa raslimali za baharini na maziwa, ili kuinua maisha ya wakazi wa Pwani na kuchangia katika kukuza pato la taifa.
Wakiongozwa na Seneta maalum Miraj Abdillah, viongozi hao wameeleza kuwa ipo haja ya haraka ya kuanzishwa kwa chuo cha mafunzo ya ubaharia katika eneo la Pwani, hatua itakayowawezesha vijana kupata ujuzi muhimu na fursa za ajira katika sekta ya baharini.
Akizungumza na wanahabari, Seneta Miraj alisema kuwa licha ya Pwani kuwa na raslimali nyingi za bahari, vijana wengi bado wanakabiliwa na ukosefu wa ajira na kutokuwa na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya eneo hilo.
Viongozi hao pia wameitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa wavuvi wanapatiwa vifaa vya kisasa, ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao za kila siku za uvuvi.
Kwa pamoja, walisisitiza kuwa sekta ya uchumi wa buluu ina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya watu wa Pwani, iwapo itawekewa vipaumbele vya kimkakati na uwekezaji wa kutosha kutoka kwa serikali zote mbili—kaunti na taifa.
Business
KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa
Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.
Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
Business
Wakulima wa Mananasi Magarini walilia soko
Wakulima wa matunda aina ya nanasi katika eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi wanaitaka serikali kuwatafutia soko ili kuuza bidhaa zao ambazo zinaendelea kuharibika msimu huu.
Kulingana na wakulima hao hakuna soko ambapo wanaweza kuuza bidhaa hizo kwa bei nzuri hali inayofanya wakulima wengi kuuza kwa bei ya chini ili kuepuka kuharibika kwa katunda hayo.
Wakizunumza na cocofm wakulima hao walisema kuwa kwa sasa wanakadiria hasara kwani matunda ni mengi.
Wakati huo huo wakulima hao wameitaka serikali ya kaunti kujenga viwanda.
Ni kauli ambayo imeongwa mkono na wafanyibiashara wa matunda mjini Kilifi kaunti ya Kilifi ambao walisema kuwa matunda mengi msimu huu huharibika kutokana na idadi ndogo ya wateja.
“Serikali itutafutie soko pamoja na kujenga viwanda ili kusaidia wakulima na wafanyibiashara wa matunda aina ya mamanasi, kuuza matunda yao ili kuawaepushia hasara hasa wakati huu ambapo matunda ni mengi.”
Taarifa ya Pauline Mwango

