Business
Kenya Yapiga Hatua Kubwa Katika Kuboresha Uchumi wa Bahari na Maziwa – Wadau Wasema
Washikadau katika sekta ya uchumi wa rasilimali za baharini na maziwa katika ukanda wa Pwani wamesema kuwa Kenya imepiga hatua kubwa katika juhudi za kuimarisha sekta hiyo muhimu ya kiuchumi.
Wakizungumza na vyombo vya habari, wadau hao walieleza kuwa serikali imeonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha uchumi wa buluu kupitia uwekezaji katika mafunzo ya kitaalamu pamoja na usambazaji wa vifaa vya kisasa vinavyowawezesha wavuvi na wafanyabiashara wa baharini kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Aidha, washikadau hao wameitaka serikali kupitia idara husika kuwawezesha vijana zaidi kushiriki kikamilifu katika sekta ya uchumi wa bahari, wakisisitiza kuwa kundi hilo lina mchango mkubwa katika ukuaji endelevu wa sekta hiyo.
Wakati huohuo, wameitaka serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu ili kuimarisha maisha ya jamii zinazotegemea bahari na maziwa kwa riziki.
Business
Bei za mafuta kuongezeka katikati ya mwezi aprili
Kenya sasa inakabiliwa na hatari ya kupanda kwa bei za mafuta, huku mgogoro unaoendelea mashariki ya Kati ukianza kuathiri bei nchini.
Serikali sasa imeonya kuwa kufikia katikati ya mwezi Aprili, bei za mafuta huenda zikapanda ikionya kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwa sasa haliwezi kuepukika kufuatia kupanda kwa bei za mafuta kimataifa.
Waziri wa hazina kuu ya kitaifa John Mbadi aliwahakikishia wakenya kuwa hakuna cha kuhofia kwani wameweka mikakati kupunguza athari zake.
Ili kupunguza athari za bei za mafuta kuongezeka, serikali ilisema itatumia shilingi bilioni 17 kutoka mfuko wa ada ya uwekezaji wa mafuta kusaidia kudhibiti bei kwa mda wa miezi 3 ijayo.
Kwa sasa serikali inasema kuna akiba ya kutosha ya mafuta na shehena zaidi zinatarajiwa nchini hivi karibuni.
Taarifa ya Joseph Jira
Business
KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa
Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.
Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

