Business
Wafanyabiashara Kilifi Walalamikia Ubomozi wa Vibanda Kupisha Ujenzi wa Barabara
Wafanyabiashara katika eneo la Misufini kuelekea Kwa Mwango, mjini Kilifi, wameelezea hofu yao kuhusu hatma ya biashara zao kufuatia tangazo la serikali ya kaunti ya Kilifi la kubomoa vibanda katika eneo hilo ili kupisha ujenzi wa barabara mpya.
Wakiongozwa na Isaac Thomas, mfanyabiashara wa bidhaa za rehani, wamesema kuwa mpango huo wa ubomoaji utasababisha hasara kubwa kwao, hasa kupoteza wateja wa kudumu, jambo ambalo linaweza kusambaratisha kabisa biashara zao.
“Biashara hii ndiyo tegemeo langu pekee. Nikiondolewa hapa bila mpango mbadala, nitapoteza wateja wangu na maisha yatakuwa magumu,” alisema Thomas.
Wameiomba serikali ya kaunti kuwapatia eneo mbadala la kufanyia biashara kabla ya kutekeleza zoezi hilo la ubomoaji, wakisisitiza kuwa wengi wao hutegemea biashara hizo kwa riziki ya kila siku.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa serikali ya kaunti, barabara inayopangwa kujengwa kutoka Misufini hadi Kibaoni inapita katika kiwanja kinachomilikiwa na Chuo Kikuu cha Pwani, hali inayowalazimu kuondoa miundo mbinu isiyo rasmi ili kuwezesha ujenzi huo.
Wafanyabiashara sasa wanasubiri kauli ya mwisho kutoka kwa mamlaka husika kuhusu mustakabali wao.
Business
Wafanyibiashara wa mitumba eneo la Diani wafunga biashara zao
Wafanyibiashara wa mitumba katika soko la Diani, kaunti ya Kwale, wamelazimika kufunga biashara zao kutokana na kudorora kwa shughuli za kibiashara katika kipindi hiki cha msimu wa watalii wachache na mvua zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Wafanyabiashara hao wanasema idadi ya wanunuzi imepungua kwa kiasi kikubwa, hali iliyosababisha nguo nyingi kukosa soko.
Kulingana na wafanyibiashara hao wanategemea zaidi watalii wa ndani na nje na kutokana na msimu huu kuwa uko uko chini wateja wamepungua hali inayofanya maisha kuwa mgumu.
Wanasema wamelazimika kutupa baadhi ya nguo kwani zimesalia sokoni kwa muda mrefu hadi zingingine kuharibika, jambo ambalo limepelekea kupata hasara kubwa.
Aidha, wameongeza kuwa bei ya nguo za mitumba imeendelea kupanda ambapo wananunua ngunia moja kwa shilingi elfu 40 huku mauzo yakizidi kushuka.
“ Biashara imedorora sai kwani hakuna wateja ikizingatiwa kuwa tunategemea sana watalii na sasa hakuna wageni hata imetulazimu kutupa nguo kwani ngigi zimeharibika baada ya kukaa kwa mda mrefu bila kununuliwa”.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
Mamlaka ya AFA yahimiza upanzi wa mkorosho
Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini AFA, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taifa linaboresha mazao yake na kuchangia uzalishaji wa chakula nchini.
Hatua hii imechangia zaidi na mikakati endelevu ya kuwawezesha wakulima kufahamu mipango endelevu ya uimarishaji wa Kilimo cha sasa na kwa kuzingatia utumiaji wa mifumo bora ya kilimo.
Mamlaka hiyo ambapo inaendeleza kampeni ya kuhamisha wakulima kuhusu umuhimu wa kilimo cha Korosho imesisitiza haja ya ujumuishaji wa wakulima, wawekezaji na wadau mbalimbali ili kupiga jeki sekta ya Kilimo huku ikiahidi kuendeleza hamasa kwa jamii za kaunti za Pwani kuhusu kilimo cha korosho na utafutaji wa soko huru.
Katika Kongamano la kitaifa lililoandaliwa katika kaunti ya Kwale, Mamlaka hiyo iliwapa wakulima kutoka kaunti sita za Pwani miche ya mikorosho elfu mia moja katika juhudi za kukuza kilimo cha zao hilo nchini.
Katibu katika Idara ya Kilimo nchini Paul Kiprono, alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Kiprono alitoa wito kwa serikali za kaunti pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kushirikiana kwa karibu ili kuboresha kilimo cha korosho.
“Kenya ilikuwa ikiongoza katika zao la mkorosho katika miaka ya 1990 lakini kutokana na changamoto za kibiashara zao hilo lilishuka katika masoko ya kimataifa kutokana na ukosefu wa kuwekezaji kwa wakulima lakini sasa tumeanza kupiga hatua kwani tunazalisha zaidi ya tan elfu 9 za korosho”, alisema Rono.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AFA, Cornelly Serem, alisema mamlaka hiyo imejizatiti kuboresha kilimo cha korosho kupitia utoaji wa miche bora na mafunzo kwa wakulima ili kuongeza tija.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

