News
Mauaji ya wazee kwa shutma za uchawi yapungua Rabai-Kilifi.
Idara ya usalama kaunti ya Kilifi imetaja kupungua kwa visa vya mauaji ya wazee wanaohusishwa na tuhma za uchawi katika eneo bunge la Rabai.
Naibu Kamishna wa eneo hilo Joseph Lenkarie alikiri kuwa visa hivyo vilikuwa vimekithiri eneo hilo huku akiwahimiza wakaazi kuendelea kuzingatia usalama wa wazee.
Wakati huo huo aliwataka maafisa wa utawala wa mkoa eneo hilo kuhakikisha mradi wa usambazaji umeme mashinani unatekelezwa ili kuwafaidi wananchi.
“Yale maneno tulikuwa tunapiga wazee ni ukweli tumeacha, sini ukweli ama bado mnapiga wazee? ya pili nimeambiwa tuliletewa umeme, wale machifu miradi ya stima inafanyika kwenu, lazima mjue yale mambo watu wa Kenya Power walisema na ni lazima tujuwe kama wamefanya hiyo kazi hatutaki kudanganya wananchi”, alisema Lenkarie.
Alisema ni jukumu la machifu kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu miradi yote iliyoanzishwa na serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati huku akiwaonya wote watakaozembea katika majukumu yao.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

