News
Rais Ruto atia saini Miswada miwili kupiga jeki Mgao wa Serikali za Kaunti
Rais William Ruto ametia saini na kuwa sheria miswaada miwili muhimu inayokusudiwa kupiga jeki ufadhili wa Serikali za Ugatuzi nchini.
Rais Ruto ambaye anahudhuria Kongamano la Ugatuzi mwaka huu katika kaunti ya Homa Bay, ametia saini mswada kuhusu Ugavi wa pato la serikali kwa hazina za Kaunti wa 2025, na pia Mswada mwengine unaotoa muongozo wa matumizi ya fedha za serikali za Kaunti wa 2023.
Mswaada unaohusu usimamizi na muongozo wa matumizi ya pesa za kaunti sasa umefutiliwa mbali na kubuni Hazina ya mabunge ya Kaunti zote 47.
Mswaada huo wa nyongeza ya pato kwa kaunti umeongoza kiwango cha hapo awali kutoka Shilingi billioni 387.4 mwaka uliopita hadi kiwango cha Shilingi bilioni 415 katika kipindi cha mwaka huu 2025/26 cha matumizi ya pesa serikalini.
Hafla hiyo ya kutia saini miswaada hiyo miwili,imefanyika katika Ikulu ndogo kaunti ya Homabay Jumatano Agostu 13 2025.
Mswaada huo uliowasilishwa bungeni na Senta wa Meru Kathuri Murungi, unayapa uhuru zaidi Mabunge ya Kaunti katika masuala ya usimamizi wa fedha zao.

Hatua hiyo imetokea wakati Kongamano la Ugatuzi limefunguliwa rasmi katika Kaunti ya Homabay, kutathmini mafanikio na changamoto kwa serikali za Kaunti.
Kongamano hilo linahudhuriwa miongoni mwa wengine Wafanyi biashara na washika Dau mbali mbali wa kimaendeleo katika ngazi za Kaunti.
Hazina kuu ya Serikali sasa inatarajiwa kuhakikisha kuwa mgao huo wa fedha unafikia hazina za serikali za Kuanti kabla ya tarehe 15 ya kila mwezi
Katika muda wa miaka miwili iliyopita serikali kuu ya kitaifa imeshtumiwa vikali na Baraza la Magavana, kwa madai ya njama za kuhujumu Ugatuzi nchini.
Taarifa ya Eric Ponda
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

