Business
Sekta ya biashara yaimarika kaunti ya Homabay
Sekta ya biashara katika kaunti ya Homabay ambako kongamano na ugatuzi linaendelea, imeimarika hata zaidi.
Kulingana na wamiliki wa mikahawa na baa eneo hilo walisema kuwa vyumba vya kukodi vilijaa kutokana na idadi kubwa ya wageni ambao walishiriki kongamno hilo kufanya uchumi wa eneo hilo kuinuka hata zaidi.
Wakizungumza na Mwanahabari wetu ambaye anaendelea kukita kambi katika eneo hilo wamiliki hao wanasema kuwa kwa sasa pesa inazunguka kwa wingi hali ambayo imefanya uchumi kuinuka.
Aidha walisema kuwa kaunti hiyo na wageni ambao wanafanya biashara katika eneo hilo wamenufaika hata zaidi kufuatia ujio wa kongamano hilo.
Waliitaka serikali kuu na kaunti kuendelea kuekeza zaidi kwa vijana kwani wako katika nafasi nzuri ya kuinuka kiuchumi.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
Bei za mafuta kuongezeka katikati ya mwezi aprili
Kenya sasa inakabiliwa na hatari ya kupanda kwa bei za mafuta, huku mgogoro unaoendelea mashariki ya Kati ukianza kuathiri bei nchini.
Serikali sasa imeonya kuwa kufikia katikati ya mwezi Aprili, bei za mafuta huenda zikapanda ikionya kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwa sasa haliwezi kuepukika kufuatia kupanda kwa bei za mafuta kimataifa.
Waziri wa hazina kuu ya kitaifa John Mbadi aliwahakikishia wakenya kuwa hakuna cha kuhofia kwani wameweka mikakati kupunguza athari zake.
Ili kupunguza athari za bei za mafuta kuongezeka, serikali ilisema itatumia shilingi bilioni 17 kutoka mfuko wa ada ya uwekezaji wa mafuta kusaidia kudhibiti bei kwa mda wa miezi 3 ijayo.
Kwa sasa serikali inasema kuna akiba ya kutosha ya mafuta na shehena zaidi zinatarajiwa nchini hivi karibuni.
Taarifa ya Joseph Jira
Business
KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa
Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.
Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

