International News
Trump asema Marekani itasitisha vita dhidi ya Iran
Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani itaondoka Iran hivi karibuni na hatua za kijeshi za nchi hiyo zitakomeshwa ndani ya wiki mbili au tatu zijazo.
Rais Trump alisema Marekani imefikia malengo iliyojiwekea kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mwezi uliyopita kwa ushirikiano na Israel.
Aidha aliongeza kuwa lengo la kuizuia Iran kuwa na uwezo wa kuunda silaha za nyuklia limefikiwa na sasa Marekani inamaliza kazi.
Trump pia aliema Marekani sasa inatawala anga za Iran na pia imepata mabadiliko ya utawala kufuatia mauaji ya viongozi wakuu wa kisiasa na kijeshi.
Aliwataja viongozi hao wapya mjini Tehran kama walio na misimamo mikali na waadilifu zaidi, ikilinganishwa na watangulizi wao.
Trump pia alisema viongozi wa Iran wanaomba kufanya makubaliano na Marekani ili kumaliza vita, madai ambayo hapo awali yalipingwa na Iran na kuongeza kwamba vita vinaweza kumalizika bila makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Kuhusu athari za vita hasa kupanda kwa bei ya mafuta, rais Trump alisema bei itashuka mara tu Marekani itakapomaliza hatua zake za kijeshi.
International News
Bunge la Israel limepitisha sheria mpya ya adhabu ya kifo
Bunge la Israel limepitisha sheria mpya inayotoa adhabu ya kifo kwa Wapalestina watakaopatikana na hatia ya mashambulizi ya mauaji dhidi ya Waisrael.
Sheria hiyo ilipitishwa kwa kura 62 dhidi ya 48, huku mbunge mmoja akijizuia kupiga kura na wengine kutohudhuria kikao hicho.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alihudhuria kikao hicho na kupiga kura kuunga mkono mswada huo bungeni.
Mswada huo wa sheria uliwasilishwa na Waziri wa usalama wa taifa hilo Itamar Ben Gvir, ambaye ni mmoja wa wanasiasa wenye msimamo mkali nchini humo.
Hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa wa kimataifa, huku mataifa ya Umoja wa Ulaya na mashirika ya haki za binadamu yakielezea wasiwasi mkubwa.
Muda mfupi baada ya kupitishwa, kundi la haki za binadamu la Israel lilisema limewasilisha malalamiko katika Mahakama kuu ya nchi hiyo.
Mamlaka ya Palestina ilitaja mswada huo kama uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Palestina, ikisema kwamba unakiuka mkataba wa Geneva.
Hata hivyo mamlaka ya Washington ilisema kwamba Israel ina haki ya kutungu sheria zake huku nchi zikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uingereza zikielezea wasiwasi mkubwa kuhusu mswada huo.
International News
Mojtaba Khamenei kutangwa kiongozi mpya wa Iran
Iran inatarajiwa kumtangaza kiongozi mkuu mpya atakayechukua nafasi ya Ayatollah Ali Khamenei aliyeuawa wiki moja iliyopita kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel.
Mmoja wa wajumbe wa Baraza la wataalam alidokeza kwamba kuna uwezekano mkubwa mtoto wa Khamenei, Mojtaba Khamenei mwenye umri wa miaka 56, akachaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi alisema viongozi wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ndio watakaomchagua kiongozi wao na wala sio rais wa Marekani Donald Trump kama alivyodai.
Wakati vita vikiingia siku ya tisa, mashambulizi yalishuhudiwa kila upande.
Israel ilishambulia maghala na vituo vya kuhifadhi mafuta mjini Tehran huku Iran nayo ikivurumisha makombora na droni kuelekea Israel na katika nchi zingine za Ghuba.
Watu sita waliripotiwa kujeruhiwa huko Israel huku wanajeshi wawili wa Israel wakiuwa kusini mwa Lebanon.
Jeshi la walinzi wa mapinduzi wa Iran limesema lina uwezo wa kuendeleza mapigano hadi miezi sita na limeonya kuwa awamu inayofuata ya mashambulizi inaweza kuhusisha makombora ya kisasa ambayo hayajawahi kutumika katika vita.
Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump, alikataa kuondoa uwezekano wa kutuma wanajeshi wa ardhini nchini Iran, hatua ambayo inaweza kuongeza hatari ya vita katika eneo hilo.
Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo katika ibada ya Misa siku ya Jumapili tarehe 8 mwezi Machi, 2026 alihimiza kukomeshwa kwa vurugu na kuanzisha juhudi mpya ili kuendeleza mchakato wa mazungumzo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

