News
Wanaosajiliwa Kwenye Mpango wa Kazi “Majuu” Waonywa.
Waziri wa Leba nchini Dakta Alfred Mutua amewaonya vijana waliopata nafasi za ajira ughaibuni dhidi ya kujihusisha na visa vya utovu wa nidhamu.
Akizungumza wakati wa zoezi la kusajili vijana kwenye mpango wa ajira za nje nchi maarufu Kazi “Majuu” katika kaunti ya Kwale, Waziri Mutua alitaja hatua hiyo kwamba huenda ikachangia kandarasi zao kufutiliwa mbali sawa na kukabiliwa kisheria.
Mutua alidokeza kwamba kuna baadhi ya vijana ambao tayari wamerejeshwa nchini kufuatia visa vya utovu wa nidhamu
“Unaskia unawashwa unataka kuandamana, unataka kuwa mwanaharakati, unataka kuchochea ingia ndege uje hapa wikendi moja uandamane kila mahali hiyo kitu ikutoke urejee kazini, kwa sababu ukienda kufanya huko maandamano unaharibia wakenya wengine, kuna watu waliandamana huko nchi tofauti tofauti, wakenya kumi na tano wengi wakasimamishwa, wakaregeshwa nyumbani, unaandamana kwa nchi nyengine wanauliza mbona mkenya anaandamana na mganda haandamani, mbona mtanzania haandamani”, alisema waziri Mutua.
Akizungumzia suala la utumizi wa dawa za kulevya, Waziri Mutua amewataka vijana hao kukomesha uraibu huo kwani hakuna taifa linaloshabikia matumizi ya dawa za kulevya.
“Hapa utafanyia ukaguzi wa kiafya kama umekuwa ukivuta bangi, madawa ya kulevya utaanguka, hata ukikataa kupatikana hapa ukifika ng’ambo utapatikana, kwa hivyo kama unataka kwenda ng’ambo achana na bangi bwana”,aliongeza waziri Mutua.
Zoezi hilo lililenga vijana 800 kaunti ya Kwale na 3,500 eneo la pwani kwa ujumla.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

