Sports
Kocha Wa Ureno Jose Mourinho Apigwa Kalamu na Fernabache Ya Uturuki
Mkufunzi wa Ureno Jose Mourinho ametimuliwa na klabu ya Fenerbahce ya Ligi Kuu ya Uturuki baada ya michezo sita pekee tangu kuanza kwa msimu mpya.
Sababu kuu ya hatua hiyo ilikuwa ni kichapo dhidi ya Benfica Jumatano usiku, kilichosababisha Fenerbahce kukosa kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Taarifa kwenye akaunti rasmi ya Fenerbahce katika X ilisomeka: “Timu yetu ya Soka ya Kitaaluma imeachana na Jose Mourinho, ambaye amekuwa kocha mkuu tangu msimu wa 2024-2025. Tunamshukuru kwa juhudi zake kwa timu yetu hadi sasa na tunamtakia mafanikio katika taaluma yake ya baadaye.”
Mourinho, mwenye umri wa miaka 62, aliteuliwa kuwa meneja wa Fenerbahce mwezi Mei 2024, akitia saini mkataba wa miaka miwili. Hata hivyo, kipigo cha 1-0 katika uwanja wa Estadio da Luz kimefupisha muda wake nchini Uturuki.
Kwa mujibu wa jarida la michezo la Uturuki, Spor Arena, uhusiano wa Mourinho na bodi ya Fenerbahce ulikuwa na misukosuko wakati wa dirisha la usajili la kiangazi, huku kocha huyo wa zamani wa Manchester United akikosoa mkakati wa klabu hiyo.
Kocha huyo amewahi kuvinoa pia vilabu vya Chelsea,Manchester United,Spurs,Real na As Roma.
Entertainment
Arsenal Ikishinda Kombe Nitampa Main Man Rio Gari na Dadangu – Shuga Boy
Mjadala mkali umeibuka katika kipindi cha COCO Asubuhi baada ya Shuga Boy, shabiki wa Manchester United, kuweka dau zito na la kushangaza dhidi ya Main Man Rio ambaye ni shabiki wa Arsenal.
Akizungumza kwenye kipindi cha COCO Asubuhi, kinachoendeshwa na Tatu Sure—inayojumuisha Shuga Boy mwenyewe, Main Man Rio na Solomon Zully—Shuga Boy alifunguka, akidai kuwa Arsenal hawana uwezo wa kubeba hata kombe moja msimu huu licha ya matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wao.
Kwa mujibu wa Shuga Boy, mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakijipa matumaini makubwa ya kutwaa hadi vikombe vinne, lakini hali halisi uwanjani haioneshi dalili hizo. Alienda mbali zaidi na kuweka dau la kipekee kwa Main Man Rio, ambaye ni shabiki mkubwa wa Arsenal.
“Nilimwambia Main Man Rio, wakibeba kombe nitampa gari yangu. Sasa naongeza dau—wakishinda kikombe msimu huu, nitampa gari yangu pamoja na dadangu,” alisema Shuga Boy kwa msisitizo, kauli iliyozua kicheko na mjadala mkali studio.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho Arsenal wamekuwa wakionyesha ushindani mkubwa chini ya kocha Mikel Arteta, wakijijenga kama moja ya timu zinazowania ubingwa wa Premier League. Licha ya maendeleo hayo, ukosefu wa vikombe katika misimu mingi bado unawapa wapinzani wao nafasi ya kuwabeza.
Kwa upande mwingine, Manchester United nao wanapitia kipindi cha mabadiliko, wakijaribu kurejea kwenye ubora wao wa zamani waliouonyesha enzi za Sir Alex Ferguson. Licha ya changamoto, bado wana historia nzito ya mafanikio, jambo linalowapa mashabiki wao kujiamini wanapojadili soka la Uingereza.
Usiku wa leo, macho ya mashabiki yataelekezwa kwenye mchezo wa ligi kati ya Manchester United dhidi ya Leeds United—mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku Shuga Boy akitumaini timu yake itapata ushindi na kuendeleza presha kwa wapinzani wao.
Wakati mabishano yakiendelea mitandaoni na kwenye studio za redio, swali kubwa linabaki: Je, Arsenal wataweza kuwanyamazisha wakosoaji wao kwa kubeba angalau kombe moja msimu huu, au kauli ya Shuga Boy itageuka kuwa unabii?

