News
Owen, Akubali kuondoa mswada wa kuharimisha Mugoka bungeni
Naibu Rais Prof Kithure Kindiki amesema kuna matumaini ya kuondolewa kwa mswada unaolenga kuharamisha mzao la Mugoka ambao ulikuwa umewasilishwa bungeni.
Kindiki alisema hatua hiyo ni kufuatia mkutano ulioandaliwa kati ya ofisi yake, viongozi kutoka Embu wakiongozwa na Gavana wa Embu Cecily Mbarire pamoja na Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya ambaye alikuwa amewasilisha mswada huo bungeni.
Katika Mkutano huo ambao ulifanyika katika makao makuu ya Naibu rais katika eneo la Karen, Kindiki aliweka wazi kwamba zao hilo ambalo linakuzwa kwa wingi katika eneo hilo ni kati ya mazao ya kibiashara na mswada uliyokuwa umewasilisha bungeni ungeondoa zao hilo kwenye orodha ya mazao ya kibiashara nchini.
“Tumeafikiana mambo kadhaa kuhusu mswada huo kutokana na shinikizo nilizopokea kutoka kwa wakulima wa zao la Mugoka na kuafikiana kwamba Mheshimiwa Baya ataondoa mswada huo bungeni”, alisema Naibu Rais.

Naibu rais Prof Kithure Kindiki na Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya wafanya mazungumzo.
Mswada huo uliwasilishwa bungeni na Mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya akilenga kuondoa zao la Mugoka katika orodha ya mazao ya kibiashara kutokana na zao hilo kuorodheshwa kuwa kati ya mazao yenye athari kubwa kwa maisha ya binadamu na umekuwa ukiathiri vijana wengi hasa eneo la Pwani.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi.
News
Wanaomiliki silaha haramu kaunti ya Tana river waonywa
Idara ya usalama kanda ya Pwani imewaonya wananchi wanaomiliki silaha haramu katika kaunti ya Tana river.
Mshirikishi wa utawala kanda ya Pwani Paul Rotich aliwataka wanaomiliki silaha hizo kuzisalimisha mara moja kwa maafisa wa polisi katika kituoc cha polisi kiilichokaribu nao.
Akizungumza katika kikao cha kiusalama kaunti ya Tana river, Rotich alisema oparesheni ya kusaka silaha hizo imeenzishwa huku akiwaagiza machifu na manaibu wao kushirikiana na maafisa wa polisi ili kuhakikisha silaha hizo zinapatikana.
Rotich alisema zaidi ya bunduki 120 ziko mikononi mwa raia wa maeneo ya Bangale na Tana Kaskazini katika kaunti ya Tana river, akisema ni lazima zirudishwe kwa serikali.
“Tunataka zile bunduki zote mnazomiliki kinyume cha sheria mrudishe kwanza ndio tuongee mambo ingine, haiwezekana mnamiliki bunduki haramu na mnataka serikali iwalinde kwani mtaishi na majangili mpaka lini, hiyo maneno hatutakubali rudisheni bunduki ama tutaanzisha oparesheni kali”, alisema Rotich.
Hata hivyo wakaazi wa kaunti hiyo wamepongeza hatua hiyo ya serikali, wakiwarai wenyeji kukumbatia amani ili kuepuka umwagikaji wa damu katika kaunti hiyo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Mahakama kuu yamzuia Kingi na Wetangula kujihusisha na siasa
Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetangula na spika wa bunge la Seneti Amason Kingi wamepigwa breki kujihusisha na mikutano ya kisiasa.
Hii ni kufuatia amri ya Mahakama kuu inayowataka wawili hao kukoma kujihusisha na uhamasishaji wa kisiasa kwa muda wakisubiri kusikilizwa kwa ombi linalopiga shughuli zao lilowasilishwa Mahakamani na Shirika la Vocal Africa.
Jaji wa Mahakama hiyo David Mburu, alitoa amri hiyo akiagiza kuwa ombi hilo lisikilizwe kwa umakini na washtakiwa wote wawasilishiwe stakabadhi za kesi hii leo.
Katika ombi hilo, Shirika la Vocal Africa linadai kuwa ushiriki wa maspika hao katika shughuli za kisiasa unaibua maswali mazito ya kikatiba kuhusiana na uhuru wa bunge na majukumu yaliyowekwa kwa maafisa wa serikali.
Vocal Africa pia limesisitiza kuwa, ingawa kila ana haki ya kuwa na maoni ya kisiasa na kushiriki katika maswala ya kisiasa, maspika wanashikilia ofisi za kikatiba ambazo hazihitaji upendelea bali zinahitaji uhuru wa kitaasisi.
Kwa muda sasa spika Kingi na Wetangula wameonekana katika mikutano mbalimbali ya kisiasa wakipigia debe ajenda ya rais William Ruto, kinyume na Katiba inayowalazimisha maspika kuangazia masuala ya bunge na shughuli zengine muhimu za kiserikali.
Taarifa ya Elizabeth Mwende

