News
Vijana eneo la Junju, Kilifi wavuna wasipopanda
Maafisa wa Idara ya utawala wa mkoa katika wadi ya Junju kaunti ya Kilifi imeonya wakaazi wa kijiji cha Mwembetsungu dhidi ya kuendekeza visa vya wizi.
Hii ni baada ya mwanamke mmoja kunusurika kifo mikononi mwa wakaazi waliokuwa na gadhabu baada ya kumfumania akiiba mahindi kwenye shamba moja kijijini humo.
Mzee wa Mtaa kwenye kijiji hicho Elijah Mbigo alisema visa vya wizi wa mahindi kijijini humo vimekithiri mno msimu huu, huku akitaja kufikia sasa zaidi ya mashamba matano yamevamiwa na mahindi kuibiwa.
Akiongea na coco fm, Mbigo aliweka wazi kwamba tayari mikakati ya kukabiliana na wizi huo imewekwa huku akiwataka wakaazi wa kijiji hicho kushirikiana ili kuhakikisha wanaotekeleza wizi huo wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Onyo ninatoa kila siku lakini bado halijazingati kwa sababu vijana hapa niwavivu hawataki vibarua, hata wakiitwa kazi mahali hawaendi, sasa hiyo inafanya mtaa umeharibika kwa sababu ya uvivu wa vijana”, alisema Mbigo.
Kauli yake iliungwa mkono na mzee wa nyumba kumi kwenye kijiji hicho Benson Mganga ambaye alisisitiza haja ya ushirikiano miongoni mwa wakaazi huku akitaka sheria kali kuchukuliwa endapo wanaotekeleza wizi huo watapatikana.
Taarifa ya Mwanahabari wetu.
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

