News
IEBC yasikitishwa na idadi ndogo ya wanaojisajili
Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, imeeleza kusikitishwa na idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kujisajili kama wapiga kura tangu kuanza kwa zoezi hilo tarehe 29 Septemba mwaka huu.
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alisema miongoni mwa changamoto zinazokwamisha usajili, ni umbali wa ofisi za tume hiyo na mchakato mrefu wa kupata vitambulisho vya kitaifa, na propaganda kwamba uchaguzi hautakuwa huru na wa haki.
Kufikia tarehe 31 mwezi Oktoba, IEBC ilisajili wapiga kura wapya 90,020 kote nchini, huku 15,619 wakihamisha kura zao, kaunti ya Mombasa ikisajili wapiga kura wapya 3,967 pekee, ikilinganishwa na lengo la wapiga kura wapya 183,000 .
Wakati huo huo Ethekon alishinikiza wakenya kupuuza madai ya wanasiasa kwamba wataiba kura zikiwemo za chaguzi ndogo.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa tume ya IEBC, Hussein Marjan, aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kujisajili na kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.
Taarifa ya mwanahabari wetu.
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

