News
Murkomen: Serikali Kubuni Kitenga Maalum Kuchunguza Mizozo ya Ardhi Pwani
ARDHI-
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema serikali inalenga kubuni kitenga maalum cha maafisa wa usalama watakaochunguza mizozo ya ardhi katika eneo la Pwani.
Katika kikao na Wanahabari, Waziri Murkomen amesema hatua hiyo itahakikisha ardhi zote zenye mizozo zinatatuliwa kwa usawa kwani idadi kubwa ya wakaazi wa Pwani wamekuwa wakihangaishwa katika ardhi zao.
Murkomen amesema Wizara ya usalama kwa ushirikiano na ile ya ardhi nchini na jamii mashinani watahakikisha utata huo unapata suluhu la kudumu sawa na kuwawezesha wananchi kupata hati miliki za ardhi zao.
Wakati huo huo amedokeza kwamba analenga kubuni sera maalum itakayosaidia kuajiri maafisa wa usalama kila mwaka ili kuimarisha usalama wa taifa huku akiwaonya wakenya dhidi ya kushiriki ufisadi wakati wa zoezi la kusajili makurutu.
Waziri Murkomen yuko katika ukanda wa Pwani kwa ziara ya wiki moja kutathmani maswala ya kiusalama ambapo alianza na kaunti ya Mombasa kisha kaunti ya Kwale, Kilifi, Lamu, Tanariver na kaunti ya Taita taveta kabla ya kukamilisha ziara hiyo.
News
Wanaomiliki silaha haramu kaunti ya Tana river waonywa
Idara ya usalama kanda ya Pwani imewaonya wananchi wanaomiliki silaha haramu katika kaunti ya Tana river.
Mshirikishi wa utawala kanda ya Pwani Paul Rotich aliwataka wanaomiliki silaha hizo kuzisalimisha mara moja kwa maafisa wa polisi katika kituoc cha polisi kiilichokaribu nao.
Akizungumza katika kikao cha kiusalama kaunti ya Tana river, Rotich alisema oparesheni ya kusaka silaha hizo imeenzishwa huku akiwaagiza machifu na manaibu wao kushirikiana na maafisa wa polisi ili kuhakikisha silaha hizo zinapatikana.
Rotich alisema zaidi ya bunduki 120 ziko mikononi mwa raia wa maeneo ya Bangale na Tana Kaskazini katika kaunti ya Tana river, akisema ni lazima zirudishwe kwa serikali.
“Tunataka zile bunduki zote mnazomiliki kinyume cha sheria mrudishe kwanza ndio tuongee mambo ingine, haiwezekana mnamiliki bunduki haramu na mnataka serikali iwalinde kwani mtaishi na majangili mpaka lini, hiyo maneno hatutakubali rudisheni bunduki ama tutaanzisha oparesheni kali”, alisema Rotich.
Hata hivyo wakaazi wa kaunti hiyo wamepongeza hatua hiyo ya serikali, wakiwarai wenyeji kukumbatia amani ili kuepuka umwagikaji wa damu katika kaunti hiyo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Mahakama kuu yamzuia Kingi na Wetangula kujihusisha na siasa
Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetangula na spika wa bunge la Seneti Amason Kingi wamepigwa breki kujihusisha na mikutano ya kisiasa.
Hii ni kufuatia amri ya Mahakama kuu inayowataka wawili hao kukoma kujihusisha na uhamasishaji wa kisiasa kwa muda wakisubiri kusikilizwa kwa ombi linalopiga shughuli zao lilowasilishwa Mahakamani na Shirika la Vocal Africa.
Jaji wa Mahakama hiyo David Mburu, alitoa amri hiyo akiagiza kuwa ombi hilo lisikilizwe kwa umakini na washtakiwa wote wawasilishiwe stakabadhi za kesi hii leo.
Katika ombi hilo, Shirika la Vocal Africa linadai kuwa ushiriki wa maspika hao katika shughuli za kisiasa unaibua maswali mazito ya kikatiba kuhusiana na uhuru wa bunge na majukumu yaliyowekwa kwa maafisa wa serikali.
Vocal Africa pia limesisitiza kuwa, ingawa kila ana haki ya kuwa na maoni ya kisiasa na kushiriki katika maswala ya kisiasa, maspika wanashikilia ofisi za kikatiba ambazo hazihitaji upendelea bali zinahitaji uhuru wa kitaasisi.
Kwa muda sasa spika Kingi na Wetangula wameonekana katika mikutano mbalimbali ya kisiasa wakipigia debe ajenda ya rais William Ruto, kinyume na Katiba inayowalazimisha maspika kuangazia masuala ya bunge na shughuli zengine muhimu za kiserikali.
Taarifa ya Elizabeth Mwende

