Entertainment
Ronald Fenty, Baba wa Rihanna, Afariki Dunia Akiwa na Miaka 70
Mwanamuziki maarufu duniani, Rihanna, anaomboleza kifo cha baba yake mpendwa, Ronald Fenty, aliyefariki dunia Mei 31, 2025 huko Los Angeles, Marekani, akiwa na umri wa miaka 70, baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.
Taarifa hizo za kuhuzunisha ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na kituo cha habari cha Starcom Network cha Barbado.
Ingawa chanzo rasmi cha kifo bado hakijatangazwa, vyanzo vya karibu vimeripoti kuwa Fenty aliaga dunia akiwa amezungukwa na familia yake, wakiwemo Rihanna pamoja na kaka yake mdogo Rajad Fenty, katika Hospitali ya Cedars-Sinai wakati wa saa zake za mwisho.
Kwa mujibu wa TMZ, Rajad alionekana akifika hospitalini mnamo Mei 28, na inadaiwa kuwa Rihanna pia alikuwa kwenye gari hilo, japokuwa hakuonekana kwenye picha.
Ronald Fenty alizaliwa mwaka 1954 huko Barbados na alikuwa msimamizi wa ghala. Alikuwa baba wa watoto sita, wakiwemo Rihanna (jina kamili Robyn Rihanna Fenty), Rajad, na Rorrey, aliowapata na aliyekuwa mke wake Monica Braithwaite, ambaye walitalikiana mwaka 2002.
Aidha, Fenty alikuwa na watoto wengine watatu—Samantha, Kandy, na Jamie—kutoka mahusiano ya awali. Familia ya Rihanna iliishi maisha ya kawaida katika nyumba ya kupangisha eneo la Bridgetown, ambalo sasa linajulikana kama Rihanna Drive. Ingawa uhusiano wa Rihanna na baba yake ulikuwa na changamoto nyingi, Fenty alihusika pakubwa katika kuhamasisha kipaji chake cha muziki tangu akiwa mdogo.
Kwa sasa, mashabiki, watu mashuhuri, na familia ya karibu wanaendelea kumpa Rihanna pole na kumfariji wakati huu wa huzuni kuu.
Entertainment
Arsenal Ikishinda Kombe Nitampa Main Man Rio Gari na Dadangu – Shuga Boy
Mjadala mkali umeibuka katika kipindi cha COCO Asubuhi baada ya Shuga Boy, shabiki wa Manchester United, kuweka dau zito na la kushangaza dhidi ya Main Man Rio ambaye ni shabiki wa Arsenal.
Akizungumza kwenye kipindi cha COCO Asubuhi, kinachoendeshwa na Tatu Sure—inayojumuisha Shuga Boy mwenyewe, Main Man Rio na Solomon Zully—Shuga Boy alifunguka, akidai kuwa Arsenal hawana uwezo wa kubeba hata kombe moja msimu huu licha ya matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wao.
Kwa mujibu wa Shuga Boy, mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakijipa matumaini makubwa ya kutwaa hadi vikombe vinne, lakini hali halisi uwanjani haioneshi dalili hizo. Alienda mbali zaidi na kuweka dau la kipekee kwa Main Man Rio, ambaye ni shabiki mkubwa wa Arsenal.
“Nilimwambia Main Man Rio, wakibeba kombe nitampa gari yangu. Sasa naongeza dau—wakishinda kikombe msimu huu, nitampa gari yangu pamoja na dadangu,” alisema Shuga Boy kwa msisitizo, kauli iliyozua kicheko na mjadala mkali studio.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho Arsenal wamekuwa wakionyesha ushindani mkubwa chini ya kocha Mikel Arteta, wakijijenga kama moja ya timu zinazowania ubingwa wa Premier League. Licha ya maendeleo hayo, ukosefu wa vikombe katika misimu mingi bado unawapa wapinzani wao nafasi ya kuwabeza.
Kwa upande mwingine, Manchester United nao wanapitia kipindi cha mabadiliko, wakijaribu kurejea kwenye ubora wao wa zamani waliouonyesha enzi za Sir Alex Ferguson. Licha ya changamoto, bado wana historia nzito ya mafanikio, jambo linalowapa mashabiki wao kujiamini wanapojadili soka la Uingereza.
Usiku wa leo, macho ya mashabiki yataelekezwa kwenye mchezo wa ligi kati ya Manchester United dhidi ya Leeds United—mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku Shuga Boy akitumaini timu yake itapata ushindi na kuendeleza presha kwa wapinzani wao.
Wakati mabishano yakiendelea mitandaoni na kwenye studio za redio, swali kubwa linabaki: Je, Arsenal wataweza kuwanyamazisha wakosoaji wao kwa kubeba angalau kombe moja msimu huu, au kauli ya Shuga Boy itageuka kuwa unabii?
Entertainment
Watoe Nyingi… Mimi Natoa Moja! Kauli ya King Kiba Yazua Mjadala
Staa wa Bongo Fleva Alikiba ameibua mjadala mzito kufuatia kauli yake aliyoitoa baada ya kufanya show kubwa na yenye mafanikio jijini Mwanza, nchini Tanzania.
Baada ya kupanda jukwaani na kuonesha kiwango chake cha juu cha uimbaji na burudani, King Kiba aliacha mashabiki wakizungumza zaidi si tu kuhusu show yake, bali pia kauli yake iliyokuja mwishoni mwa performance yake. Akiwa mbele ya umati mkubwa wa mashabiki, alisema kwa kujiamini:
“Watatoa ngoma nyingine na nyingine, na nyingine, na nyingine, na nyingine… halafu mimi natoa nyingine, moja tu.”
Kauli hiyo imezua tafsiri mbalimbali miongoni mwa mashabiki na wadau wa muziki, wengi wakiona kuwa ni ujumbe unaolenga tofauti iliyopo kati ya wasanii wanaotoa kazi nyingi kwa wakati mfupi na wale wanaochagua kutoa kazi chache lakini zenye ubora wa hali ya juu. Kwa muktadha huo, Alikiba anaonekana kusimama katika kundi la wasanii wanaoamini katika ubora kuliko wingi.
Kwa muda mrefu sasa, Kiba amekuwa akijulikana kwa mtindo wake wa utoaji wa muziki usio wa haraka, lakini unaolenga ubora wa juu na maisha marefu ya kazi zake sokoni. Hii ni tofauti na mwenendo wa sasa wa tasnia ya muziki wa kidigitali ambapo baadhi ya wasanii huchagua kutoa nyimbo mfululizo ili kubaki juu ya chati na kwenye algorithms za streaming platforms.
Kauli yake pia imekuja katika kipindi ambacho wimbo wake mpya Finale, aliomshirikisha Bien, unaendelea kufanya vizuri kwenye majukwaa ya kidigitali. Video ya wimbo huo imekuwa ikipata watazamaji wengi na maoni chanya kutoka kwa mashabiki wa Afrika Mashariki na kwingineko, hali inayoongeza uzito wa ujumbe wake kuwa kazi moja bora inaweza kuwa na athari kubwa kuliko nyingi zisizo na nguvu sawa.
Baadhi ya wachanganuzi wanasema kijembe hicho kimemlenga mpinzani wake wa karibu Diamond Platnumz ambaye ameachia nyimbo mbili (Happy na Joy) kwenye kipindi kifupi ambacho King Kiba kaachia wimbo mmoja unaofanya vizuri zaidi ya nyimbo za Simba.
Hata hivyo, mjadala unaoibuliwa na kauli hiyo una pande mbili. Wapo wanaounga mkono msimamo wa Kiba wakisema ubora ndiyo unaojenga legacy ya msanii. Lakini pia wapo wanaoamini kuwa katika ushindani wa sasa, consistency ya kutoa nyimbo mara kwa mara ni muhimu ili kubaki relevant kwenye soko lenye ushindani mkubwa.
Kwa mtazamo wa kina, kauli ya Alikiba si tu maneno ya jukwaani bali ni tafakari ya mkakati wake wa muziki na namna anavyoiona tasnia kwa ujumla. Inaibua swali muhimu kwa wasanii na mashabiki pia—je, thamani ya msanii ipo kwenye wingi wa kazi anazotoa, au kwenye ubora na uimara wa kazi chache anazoachia?
Hadi sasa, jambo moja liko wazi—kauli hiyo imefanikiwa kuamsha mjadala mkubwa, na kwa mtindo wa King Kiba, huenda hata hilo lenyewe ni sehemu ya mchezo wake wa kisanii.

