News
Wakaazi wa Voi wapendekeza mbinu mpya za kulipa ada za maji
Wakaazi wa kaunti ndogo ya Voi kaunti ya Taita Taveta wanapendekeza kampuni ya kusambaza maji mjini humo ya TAVEVO kubuni mbinu mpya ya kulipia ada ya maji kama ile ya kulipia umeme (Token) ili kumwezesha mteja wa maji kulipia kwa gharama anayoimudu.
Kulingana na wakaazi wengi wao wanakosa bidhaa hiyo muhimi ya maji kutokana na gharama ya juu wanayotozwa.
Walisema ikiwa kampuni hiyo ya kusambaza maji itakubali mapendekezo hayo huenda ikawapunguzia gharama ya kulipia maji.
‘’Kama tunaweza kuletewa Token wengi wetu tutaweza kulipa kwa gharama tunayoweza kumudu kuliko ile mita isome mpaka mwezi.Wengine wanashindiwa katikati wanakatiwa’’ alisema mkaazi
Wakati huo huo, wakaazi hao pia walishinikiza kampuni hiyo ya kusambaza maji ya Tavevo kubadilisha mita za zamani za maji na kuweka za plastic kama njia mojawapo ya kukabiliana na wizi wa mita hizo ambazo huwa zinang’olewa na kuuzwa kwa wanaonunua vyuma kuukuu.
‘’Sahizi tumekuwa na shida ya hizi mita, mita zang’olewa na sasa mimi nilikuwa napendekeza kama zinawezwa kubadilishwa na kuwekwe za plastiki kwa sababu inasemekana zinaibwa ziende ziuzwe kwa watu wa kununu scrap’’ aliongeza mkaazi.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Vita dhidi ya dhulma za kijinsia vyaendelezwa Kilifi
Visa vya ukatili wa kijinsia (GBV), dhidi ya wanawake na watoto katika kaunti ya Kilifi vinapoendelea kushuhudiwa, mikakati ingali inaendelezwa katika kuhakikisha vinadhibiti vilivyo.
Akizungumza baada ya kuzindua mchakato wa kuhamasisha jamii kuhusu visa hivyo, mwanaharakati na pia mwanzilishi wa shirika la Dada Yangu, Fatuma Ramadhan alisema kwa ushirikiamo na wadau mbalimbali wanalenga kuhakikisha jamii inapata elimu ya namna ya kukabiliana na ukatili huo wa kijinsia.
Fatuma Ramadhan pia alisema wanawake ndio waathiriwa wakuu wa dhuluma za kijinsia kupitia mitandao.
‘’Visa hivi vimekuwa vingi na ndio maana kuna haja ya kila mmoja kushiriki ipasavyo Katika kuhakikisha visa hivi vinadhibitiwa vilivyo na sio kuachia mashirika ya kijamii pekee’’ Alisema Ramadhan
Kwa upande wake Michael Baraka ambaye ni mhudumu wa bodaboda alisema watashirikiana katika kuripoti matukio hayo ili kudhibiti visa hivyo na kuitaka jamii kuondoa dhana kuwa vijana wa bodaboda wanahusika pakubwa katika utekelezaji wa dhuluma hizo.
‘’Kama wahudumu wa bodaboda tutashirikiana na kila mmoja kufanikisha hilo na pia kwa niaba ya wenzangu ningependa jamii iondoe dhana kuwa sisi tunahusika pakubwa katika visa vibaya’’ alisema Baraka.
Naye Shyleen Mumanyi wa shirika la Young Women Leadership Institute alisema katika kuhakikisha visa hivyo vinadhibitiwi watashirikiana pia na machifu na wazee wa nyumba kumi miongoni mwa viongozi wingine katika jamii.
Ni kauli ambayo iliungwa mkono na Abdulfah Nurein Mohamed huku akisema visa hivyo hasa kwa watoto huwa vinaongezeka zaidi wakati shule zimefungwa na kutoa wito kwa serikali ya kaunti ya Kilifi kuweka mikakati ifaayo katika kuimarisha usalama hasa katika fuo za habari na kusisitiza umuhimu wa wazee wa mtaa kujukumika vilivyo katika utendakazi wao.
Kwa kauli moja walikemea visa vya ukatili wa kijinsia pamoja na vile vya watu kupotea katika hali tatanishi na kutoa wito kwa serikali kuu kufanya uchunguzi wa visa hivyo kwa wakati na watuhumiwa wakabiliwe kisheria na pia kufanya kazi kwa karibu na mashirika yayototetea haki za wanawake.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Mikakati ya kudhibiti migogoro ya mipaka yaidhinishwa Kwale
Gavana wa kaunti ya Kwale, Fatuma Achani ametangaza kujengwa kwa jengo jipya la ofisi za utawala wa kaunti hiyo katika wadi ya Mackinnon gatuzi dogo la Samburu, ili kulinda na kukabiliana na migogoro ya mipaka baina ya kaunti ya Kwale na Taita Taveta.
Akizungumza katika makao makuu ya kaunti hiyo mjini Kwale, Gavana Achani alisema ofisi hiyo pia itasaidia kupunguza kero kwa wakaazi wa eneo hilo kutafuta huduma mbalimbali za serikali ya Kwale.
Gavana Achani pia alisema serikali ya kaunti ya Kwale inaendeleza mikakati katika kuhakikisha kuna miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kwa manufaa ya wakaazi.
‘’Kulikuwa na vita baina ya Kwale kaunti na Taita Taveta tuliposhinda katika kesi ile tukaonelea ili kulinda kabisa mikapa yetu tujenge ofisi pale Makina’’ alisema Achani.
Vilevile, gavana Achani alizungumzia suala la kugatuliwa kwa huduma mbalimbali za kaunti hiyo hadi mashinani kupitia ujenzi wa ofisi za utawala katika wadi zote 20 za kaunti hiyo ili kupeleka huduma za serikali karibu na wananchi.
‘’Tunalenga kupunguzia mwananchi huduma badala ya kuzifuata kwa kaunti anaweza kuzipata mashinani’’ aliongeza Achani
Haya yanajiri baada ya serikali ya kaunti ya Kwale kushinda kesi ya mzozo wa mipaka uliokuwepo katika eneo la Macknon kati ya kaunti ya Kwale na Taita Taveta mwezi Julai, 2024.
Taarifa ya Janet Mumbi

